Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN yatoa onyo kali vita Sudan

Sudani: Muda Wa Kusitisha Mapigano Umeongezwa, Mapigano Yanaendelea UN yatoa onyo kali vita Sudan

Tue, 2 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Martin Griffiths, mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kabla ya kuelekea nchini Sudan kwamba hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya sana kiasi kwamba imefikia kwenye hatua ya kusambaratika kabisa.

Amesema, utatuzi wa mgogoro wa Sudan hauwezi kupatikana kutokana na kuendelea vita hivyo.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akilizungumzia mara kwa mara suala la Sudan na hali yake mbaya ya kibinadamu tangu zaidi ya wiki mbili zilizopita, wakati yalipozuka mapigano ya pande zote baina ya Jeshi na Kikosi cha Radiamali ya Haraka.

Onyo la Umoja wa Mataifa kuhusu kusambaratika hali ya kibinadmau nchini Sudan kutokana na kuendelea mapigano limetokana na mambo kadhaa ukiwemo umaskini wa muda mrefu wanaoishi wananchi wa nchi hiyo.

Kwa miaka mingi nchi hiyo haina utulivu wa kisiasa na imekuwa vitani kwa miongo kadhaa hususan katika maeneo ya Darfur na kusini mwa nchi hiyo kabla ya Sudan Kusini kutangaza kujitenga na maeneo mengine ya Sudan.

Maandamano makubwa ya wananchi na ya muda mrefu nayo yamepelekea nchi hiyo kushughulishwa zaidi ya kukabiliana na maandamano hayo yaliyomg'oa madarakani Jenerali Omar al Bashir na kutoshughulikia masuala ya uchumi na hali ya kibinadamu nchini humo.

Mapigano makubwa ya hivi sasa pia yaliyoanza tarehe 15 mwezi ulioisha wa Aprili baina ya Jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye pia ni mkuu wa Baraza la Mpito la Uongozi la Sudan kwa upande mmoja na Kikosi cha Radiamali ya Haraka kinachoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo kwa upande wa pili, yameshadidisha masaibu ya wananchi wa Sudan.

Juhudi zote za upatanishi zimeshindwa kukomesha mapigano hayo ya kuwania madaraka hadi hivi sasa. Hali ya kiuchumi na kijamii nchini Sudan imezidi kuwa mbaya kutokana na mkwamo wa kisiasa huku waathirika wakuu wakiwa ni wananchi wa kawaida.

Mapigano baina ya Jeshi na Kikosi cha Radiamali ya Haraka vimeharibu mno mali za uma na kusababisha hasara iliyo vigumu kufidika. Huduma za maji na umeme zimepotea kabisa katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu Khartoum, na bado juhudi za upatanishi hazijazaa matunda ya kukomesha vita hivyo.

Jumamosi wiki hii, Wizara ya Afya ya Sudan ilitangaza kuwa, miongoni mwa madhara ya vita hivyo ni kuuawa watu 528 na kujeruhiwa wengine 599 hadi siku hiyo ya Jumamosi.

Hali bado ni tete kiasi kwamba hata makubaliano dhaifu yaliyofikiwa baina ya pande mbili kwa ajili ya kusimamisha vita, yanavunjwa mara kwa mara huku kila upande ukiulaumu upande wa pili.

Jumapili usiku, Kikosi cha Radiamali ya Haraka kilisema katika taarifa yake kwamba kimekubali kusimamisha mapigano kwa muda wa siku tatu.

Kilisema kimefikia uamuzi huo ili kuitikia miito ya ndani ya Sudan, ya kikanda na kimataifa na kwa ajili ya kurahisisha wananchi na raia wa kigeni kukusanya mahitaji yao na kuelekea kwenye maeneo salama.

Kikosi hicho kilidai pia kuwa, tangu kilipoanza kipindi cha usimamishaji vita, Jeshi la Sudan limefanya mashambulio kadhaa suala ambalo linaonesha jinsi jeshi hilo lisivyoheshimu ahadi zake.

Kikosi cha Radiamali ya Haraka kinaliita Jeshi la Sudan kuwa ni wafanya mapinduzi ya kijeshi wasioheshimu demokrasia. Kabla ya hapo lakini, Jeshi la Sudan lilitangaza kukubaliana na mpango wa taasisi ya kikanda ya IGAD wa kusimamisha vita nchini humo.

Komandi Kuu ya Jeshi la Sudan ilisema kwenye tamko hilo kwamba, Jenerali al Burhan amekubaliana na mpango wa IGAD wa kurefushwa muda wa kusimamisha mapigano kwa saa 72 nyingine.

Licha ya kuweko jitihada za kikanda na kimataifa za kuutatua mgogoro wa Sudan, lakini hali bado si shwari na hata makubaliano yaliyofikiwa nayo ni tete sana.

Mapigano ya hapa na pale yanaendelea. Mapigano hayo hayana tija nyingine isipokuwa kusababisha hasara kubwa tu kwa miundombinu na mali za umma za Sudan.

Ikumbukwe pia kuwa, mwezi Disemba 2022, kulifikiwa makubaliano baina ya asasi za kiraia zilizoongoza maandamano yaliyomng'oa madarakani Omar al Bashir kwa upande mmoja na Baraza la Mpito la Uongozi la Kijeshi kwa upande wa pili, lakini baraza hilo chini ya Jenerali al Burhan lilifanya mapinduzi mengine ya kijeshi, likavunja serikali ya kiraia, jambo ambalo limelalamikiwa vikali ndani na nje ya Sudan.

Kuendelea mapigano ya hivi sasa kunazidi tu kutia nguvu uwezekano wa majenerali wa kijeshi kukaa madarakani kwa muda mrefu zaidi huko Sudan na kuzidi kupotea matumaini ya kurejesha utawala wa raia nchini humo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live