Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN yatenga dola milioni 25 kukabiliana na mafuriko Somalia

Mafuriko Ya Somalia UN yatenga dola milioni 25 za kukabiliana na mafuriko nchini Somalia

Sat, 11 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi za masuala ya kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimesema kwamba zimetenga dola milioni 25 za Kimarekani kwa ajili ya kuanza kuwafikishia misaada wananchi walioathiriwa na mafuriko makubwa nchini Somalia. Tayari watu milioni moja na laki mbili wameripotiwa kuathiriwa na mafuriko hayo ya mara moja kwa karne ya nchini Somalia.

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanakadiria kuwa watu milioni 1 na laki 6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko ya msimu wa mvua unaoendelea hivi sasa huko Somalia ambao kila mwaka huanzia mwezi Oktoba hadi Desemba.

Taarifa hiyo imetolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) na kuongeza kuwa, hekta milioni 1 na laki 5 za mashamba zinaweza kuharibiwa na mafuriko mwaka huu nchini Somalia.

Taarifa ya OCHA pia imesema: Fedha hizi mpya zinajumuisha dola milioni 10 zilizotolewa na Mfuko Mkuu wa Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) na dola milioni 15 kutoka Mfuko wa Masuala ya Kibinadamu wa Somalia. Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia juhudi za kuzuia kupoteza maisha watu, miripuko ya magonjwa ya kuambukiza na kushughulikia uhaba wa chakula.

Baada ya kupitia kipindi kigumu cha ukame mkali, sasa Somalia imekumbwa na mafuriko makubwa ya karne

Fedha za CERF zitasaidia mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake kuwafikishia misaada zaidi ya watu 280,000, wakati dola milioni 15 kutoka Mfuko wa Kibinadamu wa Somalia zitasaidia zaidi ya watu 420,000.

Sehemu nyingine ya taarifa ya OCHA imesema: Somalia, ambayo kabla ya mafuriko hayo iliopitia kipindi kigumu sana cha ukame wa kihistoria, ni moja ya nchi nyingi ambazo zinatabiriwa kukumbwa na hatari kubwa ya mafuriko, ukame na joto kali katika miezi ijayo. Majanga hayo ya kimaumbile yanachochewa na vitu mbalimbali ikiwemo El Nino.

Kabla ya hapo Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilikuwa limetabiri kutokea mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea nchini Somalia katika kipindi cha karne moja yaani miaka 100 iliyopita na kusababisha maafa makubwa ya roho na mali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live