Umoja wa Mataifa umelaani vikali machafuko ya hivi karibuni katika jimbo la Warrap na katika eneo la Abyei ambayo tangu mwezi uliopita hadi sasa yamesababisha kuuawa makumi ya watu.
Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimetoa taarifa na kubainisha wasiwasi juu ya kuendelea kuwepo wanajeshi na makundi ya wanamgambo katika eneo la Abyei ambalo linagombaniwa na Sudan na Sudan Kusini na kusisitiza kuwa eneo hilo linapasa kuwa la kiraia haraka iwezekanavyo.
Nchi wanachama za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia zimeunga mkono ombi la Nicholas Haysom Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini na kusisitiza kuwa kuna ulazima kwa serikali ya Sudan Kusini kuchunguza mauaji hayo tajwa na mashambulizi dhidi ya raia katika eneo la Warrap na Abyei ili kudhibiti hali ya mambo. Nicholas Haysom
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeashiria nafasi muhimu ya kikosi cha kulinda amani cha umoja huo katika kuwalinda raia katika eneo la Abyei na kutangaza kuwa linaunga mkono mazungumzo na hatua zozote zitakazofanikisha kurejesha amani na uthabiti huko Abyei na hata katika maeneo mengine huko Sudan Kusini. Eneo la Abyei linalozozaniwa kati ya Sudan Kusini na Sudan tangu Sudan Kusini ipate uhuru mwaka 2011.