Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa (UN) Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatari inayoongezeka kati ya nchi hiyo na Rwanda.
Katika wiki za hivi karibuni, hali katika Jimbo la Kivu Kaskazini DRC kwenye mpaka na Rwanda imezorota zaidi, mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Bintou Keita ameliambia Baraza la Usalama kama alivyonukuliwa na AFP.
“Mivutano ya kikanda kati ya DRC na Rwanda imeongezeka zaidi, na kuongeza hatari ya makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi yanayoweza kuigusa Burundi,” amesema Keita.
Uhusiano kati ya DRC na Rwanda, ambao bado haujatulia tangu vita vya miaka ya 1990 na 2000, umedorora katika miaka miwili iliyopita kutokana na kuibuka tena kwa waasi wa M23 huko Kivu Kaskazini.
DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wanaoongozwa na Watutsi, ambao wanashikilia eneo kubwa Mashariki mwa nchi hiyo tangu kuanza mashambulizi mwishoni mwa mwaka 2021.
Kuongezeka kwa mvutano wa kikanda kunakuja wakati DRC ikitaka Umoja wa Mataifa kuharakisha kuondoka kwa walinda amani wapatao 14,000 kuanzia mwezi huu, huku kukiwa na maoni ya umma kwamba walinda amani hao hawafanyi kazi yao kikamilifu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) na Serikali walitia saini mpango wa kujiondoa ambao haukuwekwa wazi.
Waraka huo unaonyesha awamu ya kwanza ambayo walinda amani wangeondoka katika Jimbo la Kivu Kusini ni Aprili 30.