Umoja wa Mataifa umewataka viongozi wa kijeshi nchini Mali kuwaruhusu wachunguzi wa umoja huo kutembelea mji wa Moura baada ya taarifa za mauwaji ya raia.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa Sahel, El-Ghassim Wane, ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa mamlaka nchini Mali bado haijaruhusu uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ya licha ya mazungumzo ya kina na viongozi hao.
''Ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitafuta ufikiaji wa eneo hilo na uliweza kufanya uchunguzi wa safari ya ndege mnamo Aprili 3. Idhini ya kuwasilisha tume ya pamoja bado haijatolewa. Tunafuatilia ushirikiano wetu wa kina na mamlaka ya kitaifa ili kutatua tatizo hili."
Jeshi la Mali lilitangaza mnamo Aprili 1 kwamba limewaua wanamgambo 203 huko Moura, katikati mwa Mali, wakati wa operesheni mwishoni mwa mwezi Machi. Hata hivyo, tangazo hilo lilifuatia ripoti za mitandao ya kijamii zilizosambazwa kwa wingi kuhusu mauaji ya raia katika eneo hilo.
Shirika la kimataifa la kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema wiki hii kwamba jeshi la Mali liliua raia takriban 300 katika mji wa Moura. Shirika hilo limeripoti kuwa baadhi ya watu katika mji wa Moura, ambao wanajeshi waliwachukulia kuwa wapiganaji wa itikadi kali, waliuawa kwa maksudi. Eneo hilo ni moja ya maeneo yanayokabiliwa na vurugu kubwa katika kanda ya Sahel.
El-Ghassim Wane amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, umeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia, kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria, mauaji, unyanyasaji na kutoweka kwa lazima katikati mwa Mali tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Urusi imetoa kile kinachoelezwa rasmi kama wakufunzi wa kijeshi kwa Mali, ambayo imekuwa ikipambana na mzozo wa kikatili wa wanajihadi tangu mwaka 2012. Marekani, Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi zinasema wakufunzi hao ni wahudumu wa kampuni ya ulinzi ya kibinafsi ya Urusi ya Wagner.