Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN hatimaye yakubali kuondoa askari wake DRC baada ya miongo 2

UN MAUJAI DRCCCCC UN hatimaye yakubali kuondoa askari wake DRC baada ya miongo 2

Thu, 23 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umoja wa Mataifa umesaini makubaliano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu kuondoka kwa ujumbe wa umoja huo wa kulinda amani nchini humo (MONUSCO).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo DR, Christophe Lutundula ambaye ameeleza kuwa, makubaliano yaliyosainiwa baina yake na Mkuu wa MONUSCO yanaashiria mwisho wa ushirikiano wa pande mbili ambao umeshindwa kuzaa matunda mashariki mwa DRC kwa zaidi ya miongo miwili.

Lutundula amesema mpango wa marekebisho ulioandaliwa na serikali ya DRC kuhusu kuondoka kwa MONUSCO unalenga kuondoa mvutano unaoongezeka kila uchao kati ya kikosi hicho cha UN na raia, na kuepuka kujirudia kwa matukio ya ghasia na maafa yatokanayo na shinikizo la kuondoka kwa askari hao.

Hata hivyo makubaliano hayo baina ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na MONUSCO hayajaashiria chochote kuhusu tarehe au muda wa kuondoka kwa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa DRC. Maandamano ya Wakongomani dhidi ya uwepo wa MONUSCO nchini humo

Mara kwa mara wananchi wa Kongo DR wamekuwa wakiandamana kulalamikia kikosi hicho cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuwalinda katika kipindi cha miongo miwili cha kuweko kwao nchini humo, na kila leo mauaji ya raia yanaendelea kufanywa na magenge yenye silaha hasa katika maeneo ya mashariki mwa DRC.

Akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema kuwa, "Tunaomba kutekelezwa kwa ombi letu la kuongeza kasi ya kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

Aidha Disemba 2022, wakazi wa mji wa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu ya Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliandamana kulalamikia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupiga kura kwa kauli moja na kuongeza muda wa kuhudumu kikosi cha MONUSCO nchini humo hadi Disemba 20 mwaka huu 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live