Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN: Zaidi ya watu 41,200 wamekimbilia Ethiopia kutokea Sudan

Idadi Ya Wakimbizi Wa Ndani Nchini Sudan Yafikia 700,000 UN: Zaidi ya watu 41,200 wamekimbilia Ethiopia kutokea Sudan

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) imesema kuwa, idadi ya watu waliokimbilia Ethiopia kutokana na hali mbaya ya vita baina ya majenerali wa kijeshi inayoendelea nchini Sudan imeshapindukia 41,200.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni kabisa, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema: "Inakadiriwa kuwa, hadi tarehe 6 mwezi huu wa Juni, zaidi ya watu 41,200 walikuwa wameshavuka mpaka wa Sudan na kuingia Ethiopia, wengi wao ni Waethiopia waliorejea nyumbani.

Taarifa ya shirika la UNOCHA pia imesema, idadi kubwa ya watu wanaomiminika mtawalia nchini Ethiopia, inakadiriwa kuwa ni kati ya 700 hadi 1,000 kwa siku na hiyo ni changamoto kubwa kwa taasisi zinazofanya juhudi za kuwahudumia watu hao ambao wengi wao wanafikia kwenye kituo cha Metema katika jimbo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia.

Taarifa hiyo imetahadharisha kuwa, zaidi ya wakimbizi 4,000 wanaotafuta hifadhi na takriban 80 wanaorejea makwao wamekwama katika kituo cha Metema na kusababisha mrundikano mkubwa wa watu ambao unaweza kuwaweka katika hatari za kiafya na kiulinzi.

Kwa mujibu wa UNOCHA, zaidi ya Waethiopia 19,500 waliorejea nchini kwao kutokea Sudan wamepatiwa huduma za usafiri kutoka Metema hadi maeneo yao.

Limesema, msaada wa chakula cha moto, maji ya kunywa na huduma za afya zinatolewa katika kituo cha Metema na eneo la muda la Mandefro Terara, ni kidogo mno kuweza kukidhi ukubwa wa mahitaji ya watu hao.

Sudan imetumbukia kwenye mapigano makali ya silaha kati ya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka hasa katika mji mkuu wa Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15 mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live