Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa makumi ya watu waliuawa katika jimbo la Darfur Kusini nchini Sudan kati ya Agosti 11 na 16. Mapigano ya kuwania madaraka nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya Jeshi na vya Usaidizi wa Haraka; na juhudi za upatanishi wa kimataifa za kumaliza vita na mapigano hayo na kuzileta pande zinazozozana kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa hazijazaa matunda.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini Sudan OCHA imetangaza katika taarifa yake kwamba kuanzia Agosti 11 hadi 16, watu 60 waliuawa na 250 walijeruhiwa katika mapigano kati ya jeshi na vikosi vya usaidizi wa haraka katika jimbo la Darfur Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF yameanza tena katika mji wa Nyala katika jimbo la Darfur Kusini, na kusababisha takriban watu 50,000 kuyahama makazi yao katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kutokana na mapigano yaliyozuka Al-Zain, makao makuu ya Darfur Mashariki, ugawaji wa bidhaa za chakula na za huduma za afya na maji safi ya kunywa pamoja na malori yaliyokuwa yakielekea mji wa Nyala vimeahirishwa shughuli zao tangu Agosti 14.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu nchini Sudan pia imetangaza kuwa Hospitali ya Al-Turki inakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi na vifaa vya matibabu..