Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN: Watu 400,000 wakimbia makazi yao Sudan

Maelfu Wanatoroka Mauaji Mapya Ya Kikabila Huko Darfur Nchini Sudan UN: Mgogoro Sudan umelazimisha zaidi ya watu 400,000 kukimbia makazi yao

Sat, 2 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mapigano makali ya miezi kadhaa kati ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili hasimu, yaani Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yamewalazimisha zaidi ya watu 400,000 kukimbilia Sudan Kusini.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, takriban watu 406,356 wamevuka mpaka na kuingia Sudan Kusini tangu mapigano yalipoanza Aprili 15 huko Sudan.

Miongoni mwa wakimbizi hao wa Sudan ni wale 13,130 walioingia nchini humo kati ya Novemba 18 hadi Novemba 24.

Asilimia 93 kati yao wameingia Sudan Kusini kwa kupitia maeneo manne ya Jimbo la Upper Nile la Sudan Kusini.

Sehemu moja ya taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa na ambayo ndiyo ya karibuni kabisa imesema: "Kati ya hao, asilimia 88 ni wakimbizi wa Sudan Kusini walikuwa wamekimbilia Sudan na sasa wamerejea nchini kwao, na asilimia 12 ni wakimbizi wa Sudan.

Hali hiyo inaonesha kupungua wakimbizi wa Sudan wanaoingia Sudan Kusini ikilinganishwa na wiki za hivi karibuni."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, vyakula kama biskuti zenye nishati nyingi, vyakul vya asili na misaada ya fedha taslimu zimeendelea kutolewa kwa wakimbizi hao ili kukidhi mahitaji yao ya dharura ya chakula na lishe, kila wanapowasili. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya OCHA imesema: "Washirika wetu wanaendelea kutoa msaada wa chakula wa miezi miwili au mitatu kwa wanaorejea katika maeneo yao.

Tangu kuanzishwa zoezi hilo mwezi Septemba hadi hivi sasa, zaidi ya watu 125,000 wamepokea mgao huo wa chakula." Kwa upande wake Umoja wa Mataifa umesema: "Mapigano yanayotokana na uchu wa madaraka kati ya majenerali wa kijeshi huko Sudan yalishaua watu wapatano 9,000 hadi mwezi Oktoba, na kupelekea zaidi ya milioni 6 wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan huku watu milioni 25 wakihitaji misaada ya dharura."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live