Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN: Serikali za kijeshi si jawabu la changamoto za uongozi

Un Kijeshi Nserikali UN: Serikali za kijeshi si jawabu la changamoto za uongozi

Fri, 1 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kabla ya kuanza ziara yake barani Afrika, Asia na Amerika, na kusema kuwa serikali za kijeshi si suluhisho akiashiria mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi yaliyogubika bara la Afrika katika miezi ya hivi karibuni.

Nchi hizo ni Gabon hivi karibuni, Burkina Faso, Niger na Mali. Akizungumza Alhamisi, Guterres amesema “hebu nianze na maneno machache kuhusu mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi ambayo tumeshuhudia miezi ya hivi karibuni barani Afrika. Nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto za utawala. Lakini serikali za kijeshi si jawabu.”

Amesema badala yake serikali hizo huongeza zaidi matatizo. “Haziwezi kutatua janga, bali zinazidi kuyachochea.”

Ni kwa mantiki hiyo Guterres amezisihi nchi zote zilizokumbwa na mapinduzi ya kijeshi, zisonge mbele kuanzisha taasisi halal iza kidemokrasia na utawala wa kisheria.

Guterres amesema ziara yake inaanza leo Ijumaa ikiwa ni kiashiria cha mwezi wa diplomasia ya kimataifa, New York Marekani na duniani kote.

Amesema, “Kadri maandalizi yanavyopamba moto kwa ajili ya Wiki ya Vikao vya Ngazi ya Juu vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nitakuwa ninasafiri kwenda Kenya kushiriki mkutano wa Afrika kuhusu Tabianchi, mkutano wa ASEAN na UN wa viongozi wa serikali na nchi huko Indonesia, mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa (G20) huko India na hatimaye mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 77 (G77) nchini Cuba na kisha safari nchini China.”

Guterres amesema akiwa katika Mkutano wa Afrika kuhusu Tabianchi atamulika maeneo mawili kuhusu tabianchi.

Mosi nchi za Afrika hazijachangia katika ongezeko la joto duniani lakini “ndio ziko mstari wa mbele zikiathirika zaidi na madhara ya tabianchi ambayo ni mafuriko vimbunga na ukame.

Pili, “serikali nyingi za Afrika zina azma ya kuwekeza kwenye nishati endelevu na rejelezi wakati rasilimali nyingi za sola, upepo, maji na madini mengine zimesheheni kwenye nchi zao. Hata hivyo amesema kiwango cha juu cha madeni na riba kubwa vinakwamisha uwezo wao wa kupata fedha.

Hivyo amesema kuna haja ya kufanyika juhudi za kimataifa kwa ajili ya kuiweka Afrika latika mstari wa mbele wa mapinduzi ya nishati rejelezi na safi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live