Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) imesema akuwa, mishtuko ya mara kwa mara inayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa inatilia mkazo wajibu wa kuweko uwekezaji mkubwa zaidi nchini Ethiopia kwa ajili ya kulinda mazingira na hali ya hewa.
Ofisi hiyo imesema hayo kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuongeza kwamba, nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imeathiriwa pakubwa na hatari zinazohusiana na hali ya hewa. Tangu mwaka wa 2020, nchi hiyo imekumbwa na ukame wa muda mrefu uliotokana na uhaba wa mfululizo wa mvua hasa maeneo ya kaskazini, kusini mashariki na kusini mwa Ethiopia.
Taarifa hiyo ya ofisi ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, ukame wa hivi sasa umeathiri maeneo tofauti ya Ethiopia kama ulivyoathiri takriban watu milioni 24, wakiwemo zaidi ya milioni 11 wanaohitaji msaada wa chakula. Ramani ya Ethiopia
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali ya Ethiopia imeripoti kutokea vifo visivyopungua 57 kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo na kuathiri zaidi ya watu milioni 1.5. Zaidi ya watu 600,000 kati yao wamekimbia makazi kwenye mikoa saba kati ya 12 ya Ethiopia.
Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya UNDRR imesema pia kuwa, Ethiopia ni moja ya nchi 30 zilizoko katika hatari kubwa ambazo zinatambulia na ofisi hiyo. Imeongeza kuwa, Ethiopia hivi sasa inajitahidi kutekeleza kivitendo malengo yake ya kujiepusha na majanga ya baina ya mwaka 2023 hadi 2030.
Hivi karibuni ofisi hiyo ya UNDRR imeshirikiana na Tume ya Kudhibiti Hatari ya Maafa ya Ethiopia (EDRMC) na timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo, kukusanya zaidi ya wataalamu 60 wa kiufundi kutoka katika mashirika 25, na mikoa 12 ya Ethiopia kwenye zoezi la kuainisha awamu inayofuata ya utekelezaji wa ramani ya njia ya kupunguza maafa huko Ethiopia.