Mashirika ya kibindamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini yametahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la watu wanaorejea na wakimbizi wanaokimbia mzozo na kuelekea kaskazini nchini Sudan.
Kwa mujibu wa mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, idadi ya watu wanaowasili Sudan Kusini iliongezeka mwezi Oktoba kwa angalau asilimia 50 ikilinganishwa na mwezi Septemba.
Kufikia juzi Jumatano tarehe 8 Novemba, zaidi ya wanaume, wanawake na watoto 366,000 walikuwa wamerekodiwa kuvuka mpaka kutoka Sudan tangu mzozo huo uanze. Stephane Dujjaric
Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York Marekani msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, wakati mzozo huo wa Sudan unapoelekea kusini zaidi, unaweza kusababisha watu wengi zaidi kuhama, na kuweka shinikizo la ziada kwa juhudi za misaada ambazo tayari zimelemewa.
Ameongeza kuwa jumuiya ya misaada ya kibinadamu inaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha pale rasilimali zinaporuhusu, hata hivyo baadhi ya washirika wanatarajia kukosa fedha kabla ya mwisho wa mwaka huu, na Mpango wa Kukabiliana na Dharura kwa wanaorejea na wakimbizi nchini Sudan Kusini umeripotiwa kufadhiliwa kwa asilimia 14 pekee.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kwa kusema “ni muhimu kwamba wafadhili waimarishe msaada wao ili sisi na washirika wetu tuweze kutoa usaidizi wa chakula na lishe, vifaa vya kutosha vya usafi wa mazingira na kujisafi, pamoja na huduma endelevu za usafiri"..