Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UN:80% ya Wasudan Kusini wanahitaji ulinzi, msaada wa kibinadamu

Baraza La Usalama La Umoja Wa Mataifa Lataka Wanajeshi Kuuachilia Mji Wa El Fasher Sudan UN:80% ya Wasudan Kusini wanahitaji ulinzi, msaada wa kibinadamu

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayozidi kuzorota nchini Sudan Kusini, huku takriban asilimia 80 ya wananchi wa nchi hiyo wakihitaji kudhaminiwa usalama na ulinzi na vile vile kupewa msaada wa kibinadamu.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Oparesheni katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA), Edem Wosornu alikiambia kikao cha Baraza la Usalama jana Jumatano kuwa, Sudan Kusini iko katika hali ngumu ya kuongezeka kwa uhaba wa chakula, mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi na mzozo wa kiuchumi.

Huku akiitaja hali hiyo kama "dhoruba kamili ya mfadhaiko," Wosornu amesisitiza juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za haraka na madhubuti za kuzuia kuongezeka kwa migogoro hiyo.

"Bila kuchukuliwa hatua za haraka, mambo yatazidi kuwa mabaya zaidi katika wiki na miezi ijayo," amesema Wosornu ambapo amesisitiza kwamba, "Zaidi ya watu milioni 9, yaani 76% ya jamii ya Sudan Kusini wanahitaji ulinzi na usaidizi wa kibinadamu."

Wosornu ameendelea kusema: Kati ya hao, 54% ni watoto na 27% ni wanawake. Jumla ya watu milioni 7.1 hawana uhakika wa kupata chakula, ikiwa ni ongezeko la karibu watu milioni 1.5 tangu mwaka jana."

Mkurugenzi wa Kitengo cha Oparesheni katika Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadam ya UN ameongeza kuwa, watoto na wanawake milioni 2.5 wako katika hatari ya kukumbwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, idadi inayotazamiwa kuongezeka hadi milioni 2.7 kufikia Disemba mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live