Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHAGUZI KENYA: Kukithiri kwa rushwa kwa pelekea uhaba wa noti

KSH NOTI UHABA Kukithiri kwa rushwa kwa pelekea uhaba wa noti

Thu, 28 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huku uchaguzi mkuu nchini Kenya ukikaribia kufanyika Agosti 9, Waziri wa Usalama Fred Matiang'i amefichua kuwa benki nchini humo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa noti za Sh200 na Sh100 baada ya wanasiasa kuzitumia sana kuwahonga wapiga kura wakati wa kampeni.

Matiang'i aliyadokeza hayo siku ya Jumatano, wakati wa uzinduzi wa ukaguzi wa ripoti mpya kuhusu ulanguzi wa pesa na ufadhili wa ugaidi.

Waziri huyo wa Usalama amedai kwamba noti hizo zimekuwa zikitumika kwa wingi katika kampeni za wanasiasa wanaolenga kuwashawishi wapiga kura kuwachagua.

“Utawaona watu wakibeba pesa kwenye mifuko, wakiwapanga raia na kuwapa shilingi 200,” waziri Fred Matiang’i amesema.

“Kuna uhaba wa noti za shilingi 200 na noti za shilingi 100 katika benki zetu kwa sababu wanasiasa wanawahonga wanavijiji,” amewambia waandishi wa habari wakati wa kikao kifupi kuhusu utakatishaji wa fedha na ugaidi.

Waziri amewataka Wakenya kuwapigia kura viongozi ambao watapiga vita uhalifu, ili kuzuia nchi isikumbane na vifo pamoja na hasara za mali kama ilivyoshuhudiwa awali wakati wa mashambulio ya kigaidi.

“Ikiwa mtawachagua watu kama hawa wawe viongozi wenu, mnafikiria kuwa wataweka mazingira bora? Ni swali tunalotakiwa kujiuliza,” Matiang’i amesema. Amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu ujao una umuhimu kuhusiana na uamuzi utakaochukuliwa, ili kutatua matatizo ya ulanguzi wa fedha na ufadhili wa makundi ya kigaidi.

“Inapasa tuzingatie kupigia kura serikali itakayopiga vita ulanguzi wa pesa, la sivyo hatutafikia malengo yetu ikiwa tutachagua serikali isiyo na maadili, na ambayo haiwezi kukabiliana na ufisadi," Waziri huyo ameongeza kusema.

Mwezi ujao, wananchi wa Kenya watashiriki katika uchaguzi wa kumchagua rais mpya, wabunge, maseneta, wawakilishi wa wanawake, magavana wa kaunti na wajumbe wa mabunge ya kaunti.

Uchaguzi wa Kenya unaotarajiwa kugharimu dola bilioni 3 katika matumizi ya jumla unatarajiwa kuwa ghali zaidi barani Afrika kwa msingi wa gharama kwa kila mpiga kura.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live