Jeshi la limetangaza kuwa, limefanikiwa kuzuia majaribio 20 ya uhamiaji haramu kaskazini mwa nchi hiyo na kuwakamata wahamiaji 805 waliokuwa wanajaribu kuelekea barani Ulaya kinyume cha sheria..
Kwa miaka mingi, nchi za kaskazini mwa Afrika hasa Tunisia na Libya zimeshuhudia majaribio mengi ya wahamiaji haramu waliokuwa wanajaribu kufika barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.
Msemaji wa Jeshi la Tunisia, Hosam Eddin Al-Jababli amesema katika taarifa yake maalumu kwamba, waliozuiliwa ni pamoja na wahamiaji 782 kutoka nchi za Afrika Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara na 23 ni raia wa Tunisia.
Jeshi la Tunisia lilifanya operesheni za kuvunja majaribio hayo ya uhamiaji katika miji ya pwani ya Sfax, Nabeul, na Mahdia tarehe 5 na 6 za mwezi huu wa Mei.
Msemaji huyo ameongeza kuwa, hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wahamiaji hao, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.
Kwa miaka mingi, nchi za Afrika Kaskazini kama vile Tunisia, Algeria, Libya, Mauritania, na Morocco zimeshuhudia wimbi la wahamiaji haramu hasa kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara. Wahamiaji hao haramu wanahatarisha maisha yao kwa tamaa ya kufika Ulaya. Mara nyingi wahamiaji hao huishia kufa maji, kutapeliwa, kuingia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu na kupigwa mnada masokoni kama bidhaa kwa ajili ya kuwa watumwa wa watu matajiri.
Kwa mujibu wa serikali ya Tunisia, zaidi ya wahamiaji 37,000 haramu walikamatwa mwaka 2022 nchini humo.