Msemaji wa Tume Kuu ya Uchaguzi ya Tunisia amesema kuwa uchaguzi ujao wa raia wa nchi hiyo umepangwa kufanyika katika msimu wa machipuo mwakani kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2014 ambayo haijabadilishwa au kufutwa.
Hata hivyo Mohamed Tlili Mansri, ameongeza kuwa ni mapema mno kuzungumzia uchaguzi ujao chini ya kivuli cha sheria za sasa za uchaguzi za Tunisia.
Awali, Rais Kais Saied wa Tunisia alisisitiza udharura wa kuwachagua viongozi wa nchi kwa kuzingatia namna wanavyowajibika.
Rais wa Tunisia alisema katika hafla ya kumtangaza Waziri Mkuu, Ahmed Hachani, kwamba: "Kuna changamoto kubwa mbele yetu ambazo inabidi tukabiliane nazo ili kuilinda nchi na kudumisha usalama wa ndani."
Rais wa Tunisia ambaye wapinzani wake wanamtuhumu kuwa ni dikteta na kwamba ameisambaratisha demokrasia changa ya nchi hiyo, amedai pia kuwa anafanya kila linalowezekana ili kudumisha umoja nchini humo. Ameongeza kuwa kunafanyika juhudi za kuhakikisha kuwa haki na uadilifu vinapatikana na kwamba hatarudi nyuma katika njia hiyo. Rais Kais Saied wa Tunisia
Inafaa kuashiria hapa kuwa, tangu mwezi Julai mwaka 2021 Rais wa Tunisia alizuia shughuli za vyama vya kisiasa na kufanya baadhi ya marekebisho katika katiba ya nchi hiyo; masuala yaliyochangia mgogoro wa kisiasa wa sasa nchini humo.