Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumempoteza shujaa - SADC

1dd6de9a25c5dd2c01617dc6c499ad87 Tumempoteza shujaa - SADC

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JUMUIYA ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema imepoteza kiongozi mahiri na shujaa, John Magufuli kwa kanda nzima na Afrika kwa ujumla kutokana na juhudi zake za kusimamia kwa umahiri mkubwa maendeleo ya jumuiya hiyo pamoja na kuondolewa vikwazo vya kiuchumi vya Zimbabwe ilivyowekewa na mataifa ya Magharibi.

Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Stergomena Tax alisema jana kuwa, Hayati Magufuli alijitolea moyo wake wote kuhakikisha Zimbabwe ambayo imeteseka na vikwazo hivyo kwa muda mrefu inaondolewa vikwazo hivyo vilivyowekwa na mataifa ya Umoja wa Ulaya na Marekani.

Kiongozi huyo wa SADC alisema hayo wakati akisaini kitabu cha maombolezo kwa niaba ya jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JICC) kutokaana na kifo cha aliyekuwa Rais Magufuli.

Alisema Rais Magufuli alitumia muda mwingi wakati alipokuwa Mwenyekiti wa SADC kujenga hoja za umuhimu wa vikwazo hivyo kuondolewa hali iliyofanya mataifa yote wanachama wa SADC kuueleza Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa Mkutano Mkuu wa umoja huo kuwa umefika wakati Zimbabwe kuopndolewa vikwazo kwa sababu vinawatesa wananchi wa taifa hilo.

“Kuona hiyo haitoshi Hayati Magufuli alimtuma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi jijini New York kuueleza Umoja wa Mataifa kuhusu msimamo wake kama Mwenyekiti wa SADC pamoja na msimamo wa Tanzania kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vya Zimbabwe,” alisema.

Tax alisema baada ya juhudi za muda mrefu za Rais Magufuli kuueleza ulimwengu juu ya umuhimu wa kuondoa vikwazo hivyo, hatimaye juhudi hizo zimezaa matunda baada ya mataifa yote yaliyoiwekea Zimbabwe vikwazo kuanza kuviondoa taratibu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz