Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, leo mchana Agosti 24, 2022 inatarajia kufikisha vielelezo vya fomu namba 34 ambazo zilitumika kwenye uchaguzi.
Fomu namba 34A, 34B na 34C zilitumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022 kwa ajili ya kurekodi matokeo ya urais, ubunge na ugavana wa kila kituo nchini humo.
Tume ambayo kwa sasa imekuwa kwenye mgogoro wa ndani tangu makamishna wanne wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera kujitoa kuhusika na matokeo yaliyotangazwa Agosti 15,2022 na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati ambayo yalimpa ushindi wa urais William Ruto aliyepata kura milioni 7.1 dhidi ya kura milioni 6.9 alizopata Raila Odinga.
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Odinga aliyapinga akidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Chebukati huku akiwataka wafuasi wake watulie kwa kuwa tafuata mfumo wa kisheria kudai haki.
Odinga amefungua kesi ya kupinga ushindi wa Ruto katika Mahakama ya Juu ya Milimani ambako shauri hilo linaendelea na kama mahakama ikithibitisha kulikuwa na ukiukaji wa taratibu inaweza kufuta matokeo ya urais.
Hii ni mara ya pili kwa Odinga kwenda mahakamani kupinga matokeo ya urais ambapo mwaka 2017 alifanya hivyo na mahakama ilifuta matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta na kuagiza IEBC iitishe uchaguzi mwingine wa urais.
Hata hivyo, Odinga hakushiriki uchaguzi wa marudio kwa madai waliohusika na kuvuruga uchaguzi wa awali ndiyo haohao wamepewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa marudio.