Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuhuma za Ruto kutaka kumpindua Rais Uhuru

Rutoopic Data Tuhuma za Ruto kutaka kumpindua Rais Uhuru

Sun, 3 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Rais wa Kenya, Wiliam Ruto alimwahidi Raila Odinga na chama chake (ODM) nusu ya nafasi zote kubwa serikalini kama wangeshirikiana kumwondoa madarakani Rais Uhuru Kenyatta.

Junet Mohamed ni msaidizi, vilevile msiri wa Raila.

Hata sasa, Junet ndiye mratibu Taifa wa Azimio la Umoja.

Junet amesema mpango wa kumwondoa madarakani Uhuru ulipaswa kuanza muda mfupi baada ya kumalizika Uchaguzi Mkuu mwaka 2017.

Wakenya wanajua na dunia inafahamu kuwa mgogoro uliopo kati ya Uhuru na Ruto ni mapatano baina ya Rais na Raila.

Junet anaibua kitu kipya kwamba, Ruto alianza mapema kusuka mbinu za kumchomoa bosi wake madarakani.

Advertisement Junet ameeleza kuwa yeye alikuwa sehemu ya majadiliano, akiwa mmoja wa wasaidizi wa Raila, walipokea mpango wa Ruto kutaka kumtoa Uhuru madarakani kwa kupeleka bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Rais.

Kwa mujibu wa Junet, wajibu wa Raila ulikuwa kuwaongoza wabunge wa ODM kuunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na Rais, pindi ingewasilishwa bungeni, halafu wangepata nusu ya vyeo vyote vikubwa serikalini.

Akiendelea zaidi, Junet alisema baada ya Uhuru kuondolewa madarakani, moja kwa moja Ruto angeapishwa kuwa Rais wa Kenya, hivyo kuwa mtu wa pili kutoka jamii ya Wakalenjin kuongoza ofisi hiyo kubwa, tangu Rais wa pili, Daniel Moi.

Junet alisema, mpango wa kumwondoa madarakani Uhuru ulipaswa kutimia mwaka 2018 na Ruto kushika madaraka ya nchi, kisha Raila angekuwa Naibu Rais.

Ushuhuda wa Junet umekuja siku moja baada ya Ruto kutoa tuhuma kuwa Raila alitamka kumpindua Uhuru, kisha Raila kukanusha madai hayo. Ndipo Junet ameona ni wakati sahihi kwake kuweka kila kitu bayana.

Junet alisema, Ruto alipomfuata Raila kuomba ushirikiano wa kumtoa Uhuru madarakani, alieleza kwamba alishaona dalili za kusalitiwa na bosi wake huyo, hivyo akaona bora amuwahi.

Alisema, mpango huo wa kumwondoa Uhuru madarakani ulianza kukosa nguvu baada ya Mahakama Kuu kutengua ushindi wa urais wa Uhuru mwaka 2017, kwa kile kilichoelezwa kuwa Tume Huru na Mipaka (IBC), ilikiuka Katiba ilipokuwa inasimamia uchaguzi.

“Rais alipotangazwa mshindi, aliitisha mkutano na wabunge wa Jubilee (chama tawala). Mkutano ulifanyika Ikulu. Katika mkutano huo ilikuwa dhahiri kuwa fungate ya Rais na Naibu Rais ilikuwa imekwisha.

“Uhuru aliwaambia maofisa wa ngazi za juu kwenye chama chake kuwa asingechangia madaraka na yeyote. Hiyo kauli ndiyo ilimshitua Ruto kwamba haikuwa ya kawaida,” alisema Junet.

Akizidi kusimulia kilichotokea, Junet alisema baada ya Mahakama Kuu kutengua matokeo ya urais mwaka 2017, ilibidi Uhuru aahirishe mpango wake kuhodhi mamlaka yake kama Rais, kwa sababu alipaswa kushirikiana na Ruto katika uchaguzi wa marudio.

Junet alisema baada ya uchaguzi wa mara ya pili, Ruto alijiona anapitia wakati mgumu zaidi, kulingana na jinsi Uhuru alivyoweka vipaumbele vyake kwa miaka yake mitano ya mwisho madarakani.

Ni kutokana na ugumu huo alioona anaupitia, Junet alisema Ruto aliweka mkazo kwenye mazungumzo na Raila kuhusu mpango wa kumpindua Uhuru, lakini kilichomvunja moyo ni kwamba licha ya kufanya vikao vingi, Raila hakuwa tayari kupokea ofa yoyote, si yeye kuwa Naibu Rais, wala chama chake kupata nusu ya nafasi zote nyeti serikalini.

“Dili la Ruto kwetu lilikuwa zuri lakini tulitakiwa kupima kwa umakini,” alisema Junet.

“Kwa nini tufanye makubaliano kwa kubaki namba mbili wakati kiongozi wa chama chetu alikuwa ana sifa nyingi zaidi za kuwa Rais kuliko Ruto.”

Jumamosi iliyopita (Machi 26, mwaka huu), Uhuru alifanya mazungumzo na wazee takribani 3,000 kutoka Mlima Kenya, akawaeleza kuwa sababu ya yeye kutofautiana na Ruto ni jaribio la kutaka kumwondoa madarakani.

Ruto anakanusha vikali tuhuma za kutaka kumpindua Uhuru. Jumapili (Machi 27, mwaka huu), alisema: “Mimi sio mpumbavu. mlevi au kichaa ndiye anaweza kusaidia kuiweka pamoja Serikali halafu akaendelea kinyume na kupanga kuipindua”.

Kama Naibu Rais, najua nini napaswa kufanya, na kamwe sitathubutu, sijawahi kuthubutu na haitatokea mimi kufanya chochote kuiangusha Serikali yetu. Wote wanaoeneza propaganda, aibu kwao. Hamstahili chochote isipokuwa aibu.”

Kisha, Ruto alimtupia lawama Uhuru kwa kujiingiza kwenye propaganda kwa lengo la kutaka kuiharibu ngome yake aliyoijenga eneo la katikati ya Kenya.

Ruto akamweleza bosi wake: “Tunakusamehe, lakini usisambaze propaganda bila sababu. Sisi ni watu wa amani, tumenyooka, tunatii sheria na tunaamini katiba.”

Upande wa Junet, alisema Raila ndiye aliyemjulisha Uhuru kuhusu mpango wa Ruto kutaka kuipindua Serikali kwa kushirikiana na ODM. Na hiyo ni baada ya kuona mambo mengi serikalini yalikuwa yanakwama kwa sababu ya mgawanyiko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live