Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tshisekedi awanyooshea vidole wagombea wenzake

Tshesekedi Mkono Kampeni.png Tshisekedi awanyooshea vidole wagombea wenzake

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye ni miongoni mwa wanasiasa zaidi ya 20 wanaowania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika wiki moja ijayo, amewatupia lawama wagombea wenzake.

“Maadui wa nchi hii wamo miongoni mwa wagombea urais. Hivi sasa wanakuja kwenu wananchi. Muwe makini hasa katika kipindi hiki ambacho mnakaribia kufanya uamuzi wa nani awe kiongozi wenu,” amesema Tshisekedi.

Amesema hayo majuzi alipohutubia mkutano wa kampeni katika mji wa Mbujimayi uliopo Jimbo la Kasai, mahali alikozaliwa.

Katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 20, 2023, Tshisekedi anawakilisha chama tawala cha Union for Democracy and Progress (UDPS), akiwania kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili wa miaka mitano.

Mara ya kwanza Tshisekedi alipata nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2018, akimshinda Martin Fayulu, mmoja wa wanasiasa wenye nguvu DRC ambaye mwaka huu anagombea tena.

Katika mkutano huo, Tshisekedi amewahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa, iwapo atachaguliwa ataunda Serikali ambayo moja ya vipaumbele vyake itakuwa kurejesha amani Mashariki mwa DRC ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa utulivu.

Akizungumza na Mwananchi Digital kando ya mkutano huo wa kampeni, Waziri wa Habari wa DRC, Patrick Muyaya amesema kikundi cha M23 kimekuwa tishio Mashariki mwa nchi hii.

“Hadi hivi sasa hatuna uhakika iwapo wananchi wote katika eneo la Mashariki watashiriki uchaguzi huu, lakini dhamira yetu ni kuwa baada ya uchaguzi, kwa kushirikiana na juhudi za kidiplomasia zinazoendelea, tuhakikishe migogoro hii inamalizwa ili wananchi hawa nao waanze kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu,” amesema.

Mwanzo wa chokochoko?

Katika hali ambayo haikutarajiwa mgombea urais mwenye nguvu kutoka upinzani, Moise Katumbi amelazimika kukatisha kampeni zake baada ya risasi za moto kupigwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni Desemba 12, 2023.

Picha za video zilizosambaa mitandaoni zinamuonyesha mmoja wa askari polisi akiwa anavuja damu usoni baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo.

Kumekuwa na kutupiana lawama kuhusu tukio hilo, huku kambi ya Katumbi ikiwatuhumu polisi kwa kuwafyatulia risasi wafuasi wake waliokuwa kwenye mkutano huo.

Jeshi la Polisi kwa upande wake, limewalaumu wafuasi wa Katumbi kwa kutumia silaha za moto katika kundi la watu.

Polisi wanadai walinzi wa Katumbi walilazimika kufyatua risasi za moto kutawanya kundi kubwa la watu ili kuhakikisha usalama wa mgombea wao.

Bado taarifa rasmi kuhusu tukio hilo hazijatolewa na mamlaka husika.

Hii ni mara ya kwanza kwa vurugu kuripotiwa katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu tangu zilipoanza Novemba 19,2023.

Watu wengi, hasa jijini Kinshasa walionyesha kushitushwa na tukio hilo kwa sababu halikutarajiwa katika kipindi hiki cha mwisho wa kampeni.

Utulivu utakuwapo

Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana, amewahakikishia Watanzania wanaoishi hapa na wale wanaotaka kusafiri kuja DRC kwa ajili ya shughuli mbalimbali kutokuwa na hofu.

Balozi Mshana amesema hayo alipozungumza na Mwananchi Digital ofisini kwake jijini Kinshasa.

Kutokana na vurugu zinazoendelea Mashariki mwa DRC, watu wengi wamekuwa na wasiwasi, hasa kipindi hiki ambacho kampeni za uchaguzi zinaelekea ukingoni.

Balozi Mshana amesema kwa kiasi kikubwa eneo kubwa la DRC lina utulivu.

“Kuhusu hali ya usalama nchini DRC kwa jumla, katika majimbo yote 26, ni majimbo manne tu ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Mai-Ndombe ndiyo baadhi ya maeneo yake yana changamoto za usalama. Katika kukabiliana na hali hiyo Serikali ya DRC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na juhudi za kurejesha hali ya amani na usalama,” amesema.

Hata hivyo, Balozi Mshana amewaasa Watanzania walioko DRC na wale wanaotarajia kuja katika kipindi hiki kuhakikisha wanazingatia na kufuata sheria na utaratibu wa nchi mwenyeji wakati wote.

“Kwa jumla tangu kuzinduliwa kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu kumeendelea kuwapo hali ya amani na utulivu wakati wote. Wagombea wote 26 wa urais wanaendelea kufanya kampeni zao katika hali ya amani na utulivu,” amesema.

Balozi amesema, “Ni matarajio yetu kwamba hali hiyo itaendelea kuwapo wakati na baada ya uchaguzi mkuu na kutangazwa matokeo. Sisi kama nchi rafiki tunawatakia na tunawaombea uchaguzi mwema majirani na ndugu zetu wa DRC.”

Kampeni za Uchaguzi Mkuu zilizinduliwa Novemba 19,2023 na zitahitimishwa Desemba 18, huku uchaguzi ukipangwa kufanyika Desemba 20, 2023.

Wanasiasa 26 wamepitishwa na Tume ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kuwania nafasi ya urais, ingawa kuna taarifa kuwa wagombea wanne wameamua kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono Katumbi, mgombea wa upinzani mwenye nguvu kubwa kisiasa na kiuchumi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live