Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Félix-Tshisekedi ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo vya mtu binafsi na vya kimuundo kwa mamlaka ya nchi ya Rwanda na wapiganaji wa M23.
Tshisekedi ameyasema hayo Januari 30, 2023 jijini Kinshasa, wakati akitoa hotuba yake mbele ya mabalozi wa nchi za kigeni nchini humo na kuongeza kuwa Rwanda inakiuka sheria za Kimataifa kwa kufanya uhalifu na kukiuka haki za Binadamu.
Amesema, “Nasisitiza ombi la serikali ya Kongo, lililowasilishwa tangu mwezi Septemba mwaka jana kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuweka vikwazo vya mtu binafsi na vya pamoja kwa mamlaka ya Rwanda, magaidi wa M23 pamoja na taifa la Rwanda.”
Tshisekedi ameongeza kuwa, “haiwezekani kuendelea kuficha ukweli ambao tayari unajulikana kwa wote na kukataa kujadili ripoti hii, ili kuficha wahusika wa uhalifu huu bila ujinga au udhaifu, DRC inasalia kujitolea katika mchakato wa amani wa Nairobi na Luanda na inasisitiza imani yake kwa mpatanishi aliyeteuliwa.”
Aidha, Rais wa DRC amesisitiza juu ya ukweli kwamba uchokozi wa Rwanda ni kutokana na sababu za kiuchumi na vya kikatili na kusema janaa, leo, au kesho, hakuna mzalendo atakayekubali kuachia Rwanda sentimita hata kidogo ya ardhi ya DRC.
Akiongea kwenye jukwaa la Umoja wa Mataifa, Rais Tshisekedi alisisitiza kutetea uadilifu wa eneo DRC, mamlaka na uhuru wa nchi hiyo bila kujali gharama na kusema hakuna Mkongo aliyedanganyika au kuwa mjinga juu ya ukweli huo.