Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki wanaokutana mjini Bujumbura wamesema rais wa DR Congo amekubali kuongeza muda wa vikosi vya umoja huo nchini DRCongo hadi mwezi Septemba.
Akiwa Botswana mwezi uliopita, Rais wa DR Congo, Felix Tshisekedi alisema vikosi vya Afrika Mashariki vitaondoka nchini humo "ikiwa hawataonyesha matokeo mazuri"kufikia mwisho wa muhula wao leo Juni 1.
Vikosi vinavyoongozwa na Kenya vilipelekwa katika maeneo ambayo waasi wa M23 walikuwa wakiondoka wakati wakuu wa majimbo wakiendelea na juhudi za amani.
Viongozi wa DR Congo wanalalamika kuwa vikosi hivyo havikuhusika katika kupambana na waasi.
Mkutano huo uliofanyika mjini Bujumbura siku ya Jumatano ulisisitiza kuwa ukosefu wa usalama mashariki mwa Congo "unaweza kutatuliwa kwa njia endelevu kupitia mchakato wa amani ya kisiasa na mazungumzo kati ya pande zote".
Kumekuwa na usitishaji mapigano na utulivu tangu mwezi Machi wakati waasi wa M23 walipokubali kuondoka katika maeneo waliyoyateka ili kukaliwa na vikosi vya kikanda.
Zaidi ya raia laki tano wameyakimbia makaazi yao katika mkoa wa Kivu Kaskazini kutokana na mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la DR Congo.
DR Congo inaituhumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, jambo ambalo Rwanda imekuwa ikilikanusha mara kwa mara.