Ofisa wa Polisi ambaye ni trafiki anayefahamika kwa jina Kelvin Korir amefariki dunia juzi Jumamosi, baada ya kugongwa alipokuwa akiongoza magari kwenye makutano ya barabara ya Kiambu-Northern nchini Kenya.
Taarifa iliyotolewa na polisi nchini humo imeeleza kwamba, askari huyo mwenye cheo cha Konstebo, alikuwa akiyaelekeza magari kwenye makutano ambapo gari aina ya Prado lilimgonga na kufariki papo hapo.
Ripoti ya polisi imeeleza kuwa Prado hiyo iliyokuwa inaendeshwa na dereva Eric Ongoya mwenye umri wa miaka 33, ilikuwa ikitoka Nairobi kwenda Kiambu.
"Mwili umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta na gari limepelekwa katika kituo cha polisi cha Kiambu yakisubiri uchunguzi,” imeeleza taarifa ya polisi.
“Dereva Ongoya anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kiambu akisubiri kufikishwa mahakamani," ripoti ya polisi imeeleza.
Watu mbalimbali wametuma salamu za rambirambi na kuwapa pole familia ya Konstebo Korir.
John Maina Mwaniki aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii; "Huyu bwana alikuwa mtu mzuri na kuheshimika, rafiki wa wote. Mtu mzuri mwenye busara pia mtu mchapakazi nimepoteza rafiki,"
"Aliondoka nyumbani asubuhi kwenda kazini, kuona mwili wa mwenzangu akiwa amefariki, kumenifanya nitetemeke," amesema Ofisa wa Polisi Sammy Ondimu.
Wiki mbili zilizopita, ofisa mwingine wa trafiki Nairobi alifariki katika ajali mbaya baada ya lori kugonga gari alilokuwa akilikagua kando ya Barabara ya Outering.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Buru Buru, Francis Kamau alisema afisa huyo wa polisi aliaga dunia wakati alipokuwa akipelekwa hospitalini.