Mara tu habari zilipoibuka kuhusu tetemeko la ardhi la Ijumaa nchini Morocco, nchi mbali mbali duniani zilionyesha nia ya kujitolea kusaidia katika shughuli ya uokoaji.Lakini nchi hiyo hadi sasa imekuwa ikichagua kile ilichochagua kukubali.
Taarifa kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Morocco iliyotolewa siku ya Jumapili ilisema: "Katika awamu hii imeitikia vyema azma ya mataifa yaliyojitolea kutoa usaidizi kama vile : Uhispania, Qatar, Uingereza na Falme za Kiarabu".
Uhispania imetuma kikosi cha utafutaji na uokoaji na mbwa wa kunusa na Uingereza imetuma timu kama hiyo, lakini kumekuwa na maswali kuhusu ni kwanini Morocco imezorota katika kujibu kiito ya usaidizi kutoka mataifa mengine.
Msaada wa Ufaransa uko katika hali ya kusubiri lakini mkuu wa shirika moja la uokoaji, Secouristes sans Frontieres, alisema wafanyakazi wake wa kutoa misaada hawakupewa kibali kutoka kwa serikali ya Morocco, shirika la habari la AFP linaripoti.
Algeria, ambayo ilikata uhusiano wa kidiplomasia na jirani zake wa Afrika Kaskazini miaka miwili iliyopita, ilisema inaweza kutuma waokoaji 80 maalumu kutoka katika kikosi chake cha ulinzi wa raia.
Pia kumekuwa na nia za usaidizi kwa Morocco kutoka Marekani, Tunisia, Uturuki na Taiwan miongoni mwa nchi nyingine.
Lakini uamuzi wa ni usaidizi gani inayotaka kuupokea limejikita katika masuala ya uhuru na siasa za kijiografia zaidi.