Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yazidi kung’ara Afrika, Carribean

73eb6c9412fbcac213418be4d38578a4 Tanzania yazidi kung’ara Afrika, Carribean

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA imezidi kung’ara katika Bara na Afrika baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS).

Miongoni mwa sababu ya kushika nafasi hiyo ni pamoja sera nzuri na hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli katika kusimamia masuala mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Uamuzi wa kuichagua ulifanywa na mabalozi kutoka nchi 15 za ukanda wa Mashariki mwa Afrika kwenye kikao kilichofanyika Julai 2 mwaka huu na kuthibitishwa kwa kauli moja na mabalozi wote wa nchi 79 wa OACPS kupitia kikao chao kilichofanyika Brussels, Julai 14.

Inaongoza kwa kipindi cha miezi sita tangu Agosti Mosi mwaka huu hadi Januari 31 mwakani; nafasi ambayo imetokana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Abuok Nyamanga kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS waliopo Brussels.

Kulingana na utaratibu wa jumuiya, nchi inayotoa mwenyekiti wa mabalozi wa, waziri wake anayesimamia masuala husika ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, moja kwa moja anakuwa Rais wa Baraza la Mawaziri.

“Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS tangu ilipojiunga mwaka 1975,” ilisema taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Iliendelea kusema: “Miongoni mwa sababu za kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ni kutokana na kuongozeka kwa ushawishi wake kwenye Jumuiya ya OACPS, sera na hatua thabiti zinazochukuliwa na Rais Magufuli katika kusimamia masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.”

Sababu nyingine ni pamoja na utendaji madhubuti wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kusimamia Sera ya Mambo ya Nje ikiwamo ushiriki mahiri wa Tanzania katika masuala yanayogusa maslahi ya nchi wanachama wa Jumuiya.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alikabidhiwa rasmi nafasi hiyo mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri, Dk Damas Ndumbaro ndiye alipokea kwa niaba yake wakati wa mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa OACPS uliofanyika kwa njia ya mtandao Julai 28.

Tanzania ilivyojipanga

Tanzania inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gambia ikiweka bayana ilivyojipanga kutekeleza masuala mbalimbali yenye maslahi kwa jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kusimamia ukamilishwaji wa majadiliano kuhusu mkataba mpya wa ushirikiano wa nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya (EU) unaotarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani.

Mkataba huo utaanza baada ya wa sasa wa Cotonou kufikia ukomo Desemba mwaka huu. Tanzania pia imesema itahakikisha maslahi ya nchi za OACPS yanaingizwa kwenye mkataba huo mpya.

Aidha, Tanzania imejipanga kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya jumuiya katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) na madhara yake kiuchumi kwa nchi wanachama.

Maeneo mengine ya kipaumbele yatakayosimamiwa na Tanzania katika kipindi cha urais wake kwa baraza hilo la mawaziri wa OACPS ni kusimamia mikakati ya kuongeza mtangamano na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama; kusimamia mabadiliko ya kiutendaji na mifumo kuendana na wakati pamoja na kudumisha mshikamano na umoja miongoni mwa nchi wanachama.

Itakavyonufaika

Miongoni mwa manufaa ambayo nchi itapata kutokana na kuwa rais wa baraza hilo ni pamoja na kuongeza ushawishi wa nchi katika kupanga na kutekeleza mikakati, miradi na programu mbalimbali za jumuiya ya OACPS.

Programu hizo ni pamoja na zinazotekelezwa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na wabia wengine wa maendeleo kama vile kilimo, uwekezaji, biashara na ujasiriamali, mazingira, miundombinu, vijana na utamaduni.

Chanzo: habarileo.co.tz