Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yauza Burundi bidhaa za bil 600/-

10f73e035eb5aa2c8da26be19cc2b1b3 Tanzania yauza Burundi bidhaa za bil 600/-

Wed, 3 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) baina ya Tanzania na Burundi ukianza leo mjini hapa huku ajenda ya uwekezaji na biashara ikiwa ni moja ya ajenda za kipaumbele katika mkutano huo, imebainika kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Tanzania imeuza nchini Burundi bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 600.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Kanali Wilbert Ibuge alisema hayo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari na wataalamu kutoka nchi hizo mbili waliokutana jana mjini Kigoma.

Balozi Ibuge alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni ushirikiano katika masuala ya siasa, diplomasia, ulinzi na usalama, uendeshaji wa miundombinu ya uchumi, biashara, uwekezaji, maliasili, utalii, madini, elimu, afya na michezo.

Alisema pamoja na hayo, majadiliano makubwa ya mkutano yatajikita katika masuala ya kipaumbele katika biashara, uwekezaji na madini ambapo alibainisha kuwa Tanzania imefanya biashara yenye thamani ya Sh bilioni 600 kwa kuuza bidhaa mbalimbali nchini Burundi kati ya mwaka 2015 hadi 2019.

“Mkutano huu unalenga kukuza ushirikiano wa kidiplomasia, uchumi, siasa na masuala ya ulinzi na hapa tunatarajia kuendeleza masuala ya kiuchumi kwa nchi, lakini mambo yanayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Balozi Ibuge.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Burundi, Balozi Isidori Nyandwi alisema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Burundi unapaswa kuenziwa na kutunzwa kwa nguvu zote kwani umekuwa na manufaa kiuchumi, kisiasa na kuisalama kwa wananchi wa nchi hizo.

Alisema baada ya misukosuko ya vita kwa sasa Burundi imetulia na imejikita katika kujenga uchumi huku wakitumia baadhi ya mambo yanayofanywa na Rais John Magufuli katika kusimamia utekelezaji wa masuala ya serikali.

“Kwetu Raisi Magufuli amekuwa mfano wa kuigwa kwa kuchukua na kutekeleza mambo mengi ambayo Serikali ya Tanzania inafanya hivyo utaona kwamba vikao hivi kwetu ni muhimu na tumepewa maagizo maalumu na Rais Ndayishimiwe kuhakikisha tunaweka umakini mkubwa katika masuala yanayojadiliwa na mkutano huu,” alisema Balozi Nyandwi.

Alisema kulingana na mabadiliko ya taratibu mbalimbali duniani, mkutano huo ni muhimu kuangalia mabadiliko hayo na changamoto zake ili kufanya mabadiliko ya kisera na sheria ili masuala ya ushirikiano yasiwe na vikwazo.

Mkutano huo ni sehemu ya maazimio yaliyofikiwa baina ya Rais Magufuli na Rais Evarist Ndayishimiye wa Burundi katika mkutano baina ya viongozi hao uliofanyika mkoani Kigoma mwaka jana.

Chanzo: habarileo.co.tz