Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yang’ara utalii Afrika Mashariki

Fa0fba83ce9d6b06cf825b345fbb44eb Tanzania yang’ara utalii Afrika Mashariki

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Utalii Tanzania imesema dunia imefahamu ukweli kuhusu usalama wa Tanzania dhidi ya virusi vya corona, ndio maana watalii wanamiminika kwa wingi kila siku kuja kutalii na kuingiza fedha nyingi za kigeni.

Akizungumza na HabariLEO jana, Ofisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania, Francis Malugu, bodi hiyo hivi karibuni ilipokea mamia ya watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia kupitia viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mkoani Kilimanjaro.

Alisema mashirika mbalimbali ya ndege ya kimataifa yakiwamo KLM, Ethiopian Airways, Qatar Airways na la Falme za Kiarabu la Emirates, ni miongoni mwa mashirika yanayoleta watalii wengi nchini kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kutokana taifa kuwa salama dhidi ya Virusi vya Corona, Baraza la Wasafiri na Utalii Duniani (WTTC) hivi karibuni iliitambua Tanzania kama nchi salama zaidi duniani na kuipa stempu maalum inayoitambulisha kuwa na kiwango cha juu cha usalama.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, watalii wengi kabla ya kufanya uamuzi wa kutembelea nchi yoyote, huwa kwanza wanataka kujihakikishia usalama wa nchi husika kuanzia ulinzi, huduma za vyakula, malazi na usafiri, hivyo stempu hiyo inawapa uhakika wa kupata huduma hizo.

Wakati hali ya utalii ikiwa shwari Tanzania, baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimekiri kuathiriwa kwa sekta zao za utalii ambazo ndio nguzo ya mapato katika uchumi wao kutokana na virusi vya corona.

Wiki iliyopita, nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zilithibitisha kupata athari kubwa kutokana na virusi vya corona ambavyo vimesababisha anga la mataifa hayo kufungwa hivyo watalii kushindwa kuingia tofauti na ilivyokuwa kabla ya virusi hivyo kuingia.

Hali ilivyo Kenya

Bodi ya Utalii ya nchi hiyo imesema baada ya kufungua anga na uchumi wa nchi Agosti Mosi, hakuna mtalii hata mmoja ambaye ameonesha nia ya kutembelea vivutio vya nchi hiyo ikiwamo mbuga ya wanyama maarufu ya Maasai Mara iliyoanzishwa mwaka 1961.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mmiliki wa kampuni ya kusafirisha watalii nchini humo, Milton Ole Siloma, wakati akizungumza na Shirika la Habari la Aljazeera, ambapo alisema mpaka sasa ni nusu mwezi tangu anga kufunguliwa, lakini hakuna mtalii hata mmoja aliyefika nchini humo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Kenya, mpaka kufikia Agosti, mwaka jana, taifa hilo lilikuwa limepata zaidi ya watalii milioni mbili, wengi wao kutoka katika nchi za Marekani, Ulaya na China na kuingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.4.

Lakini mpaka kufikia Agosti, mwaka huu, Kenya imepata hasara ya dola za Marekani milioni 752 kutokana na athari za virusi vya corona.

Nchini Uganda

Serikali ya nchi hiyo imegeukia wananchi wake kuwahamasisha washiriki katika utalii wa ndani kutokana na athari mbaya ya virusi vya corona zilioosababisha ukosefu wa watalii kutoka nje ya nchi.

Hivi karibuni, Bodi ya Utalii ya nchi hiyo, ilisema janga la corona limesababisha kuwa na uhaba mkubwa wa watalii kutoka nje ya nchi, hali iliyoilazimisha kuangalia utalii wa ndani kama njia mbadala ya kuihuisha sekta hiyo.

Kwa mujibu wa bodi hiyo, kabla ya virusi vya corona kuingia nchini humo, Uganda ilikuwa ikipata watalii zaidi ya milioni moja, lakini baada ya kutangazwa sheria ya ‘lockdown’, watalii wamepungua kwa asilimia 22.

Hali mbaya Rwanda

Bodi ya Maendeleo ya Utalii Rwanda imesema virusi vya corona vimesababisha hasara kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na bodi hiyo baada ya kufungua shughuli za kitalii mapema mwezi huu, ilisema nchi hiyo inakadiria kuwa mapato ya utalii yatapungua kwa asilimia 50 hadi 70.

Taifa hilo ambalo utalii wake mkubwa ni sokwe wa milimani, lilipata watalii milioni 1.6 mwaka jana na kuingiza dola za Marekani milioni 498, lakini mwaka huu kutakuwa na punguzo la asilimia 70 ya ingizo hilo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kutengemaa kwa sekta hiyo kunaweza kusubiri hadi miezi 12 hadi 18 ijayo.

Chanzo: habarileo.co.tz