Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yaahidi kusaidia Burundi kuingia SADC

BURU Tanzania yaahidi kusaidia Burundi kuingia SADC

Mon, 29 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia Burundi ili ifanikiwe katika adhma yake ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, marehemu Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake.

Majaliwa aliyasema hayo juzi alipozungumza kabla ya mazishi ya Rais Nkurunziza yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ingoma uliopo Gitega nchini Burundi.

,Majaliwa alisema ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli.

“Marehemu Rais Pierre Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa ametimiza kiu yake ya Burundi kuwa mwanachama wa SADC jambo ambalo halikuwezekana, naamini Mheshimiwa Rais (Rais mteule wa Burundi Evariste Ndayishimiye) utalisimamia suala hilo hadi litimie”.

Alisema Rais Dk. Magufuli amemtuma afikishe salamu za pole kwa mke na familia ya marehemu, Rais wa Burundi na wananchi wote kufuatia kifo cha Nkurunziza kilichotokea Juni 9, 2020.

Alisema Tanzania na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao huo.

Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi kumpa ushirikiano Rais wao mpya Ndayishimiye kama walivyofanya kwa marehemu Nkurunziza.

Naye, Rais wa Burundi, Ndayishimiye alisema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura juzi asubuhi Juni 26, 2020, Majaliwa alipokelewa na Waziri Mkuu wa Burundi, Prosper Bazombaza.

Baada ya mazishi hayo Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi kabla ya kurejea nyumbani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live