MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebainisha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kwa kuwa na bei ndogo ya vifurushi vya simu.
Aidha, imeelezwa kuwa ushindani mkubwa wa kampuni za simu nchini, umesababisha watoa huduma wengi kuuza huduma za vifurushi hasa data kwa bei zisizo na uhalisia, hivyo kusababisha watoa huduma wengi kushindwa kufikia viwango vya ubora wa huduma vinavyostahili.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta TCRA, Dk Emmanuel Manasse wakati akiwasilisha taarifa kuhusu gharama na tozo za vifurushi, promosheni na ofa maalumu katika semina kwa wadau wa habari na mawasiliano kuhusu Kanuni Ndogo za Gharama na Tozo za Vifurushi, Utangazaji wa Huduma na Ofa Maalum.
Alisema katika kiwango cha bei ya data, GB moja inatozwa dola za Marekani tatu ikiwa ni nchi ya tatu kwa kuwa na kiwango cha chini SADC.
“Sio nchi yenye bei ya chini ya data GB moja, japokuwa ni ya tatu katika nchi za SADC,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ndiyo yenye bei ndogo ya data kwa nchi za SADC, ambapo GB moja ni dola za Marekani 1.29.
“Bei ya juu Tanzania kwa GB moja ya kifurushi cha data ni dola za Marekani 4.5 ikiwa ni ya chini ikilinganishwa na nchi nyingine za SADC isipokuwa DRC na Msumbiji.
Aidha, alifafanua kuhusu malalamiko mbalimbali yanayotolewa na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, ikiwamo watumiaji wa simu ndogo maarufu ‘kitochi’ kulazimishwa kununua vifurushi vya data, ambavyo hawana matumizi navyo.
Alisisitiza kuwa hakuna mtumia huduma yeyote anayelazimishwa kununua kifurushi chochote, isipokuwa kinachotakiwa ni kuangalia aina ya kifurushi kulingana na mahitaji yake na aina ya kifaa cha mawasiliano anachotumia .
“Angalia kifaa cha mawasiliano unachotumia na kifurushi unachonunua.
Katika mitandao kuna vifurushi vya dakika, dakika na ujumbe mfupi (SMS) na vile vya dakika, SMS na data ni vyema mtumiaji asome na kuchagua kifurushi kinachoendana na kifaa chake cha mawasiliano,” alisema.
Alisema TCRA ingechukua hatua, endapo watoa huduma wangeweka vifurushi vya data pekee, bila kujali watanzania wengine wanaotumia vifaa visivyowezesha matumizi ya data.
Kuhusu malalamiko ya kutokuwepo kwa ubora wa huduma za data, alieleza kuwa kumekuwepo na ushindani usio na tija baina ya kampuni za simu, hali iliyolazimisha ziuze bidhaa za ndani za vifurushi hasa data kwa bei zisizo na uhalisia na kinachonunuliwa.
“Gharama za mawasiliano zinatakiwa ziwe halisia na zimwezeshe mtoa huduma kutoa huduma zenye ubora na kuendelea kuwekeza kwenye kuboresha huduma pamoja na kupanua mtandao wake,” alisisitiza.
Kuhusu vifurushi vinavyopatikana usiku pekee, Manasse alisema hakuna mtu anayelazimishwa kutumia vifurushi hivyo na kwamba ndiyo maana kwenye kanuni watoa huduma wameelekezwa kuweka vifurushi vya aina mbalimbali ili watumia huduma wavichague kulingana na mahitaji.
Alisema mteja anatakiwa kuchagua katika vifurushi vilivyowekwa na mtoa huduma kutokana na mahitaji yake, ambapo mtoa huduma huweka vifurushi vya usiku ambavyo ni nafuu kwake kwa sababu mtandao hautumiki sana usiku na hivyo kuwa na uwezo wa kutoa uniti nyingi kwa wanaohitaji.
Kwa upande wa hoja ya watumia huduma ya kutaka TCRA kutoruhusu vifurushi vyote kuisha muda wa matumizi, bali mtumiaji kutumia kifurushi hadi mwisho wake, alifafanua kuwa kila mteja anapojiunga na kifurushi anakubali kupewa huduma aliyonunua na kwa muda uliowekwa.
‘’Vifurushi hivi haviwezi kutumika baada ya muda ulioweka kuisha hata kama havijatumika na Mamlaka imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka kanuni kadhaa ikiwemo ya kumtaka mtoa huduma kuwawezesha watumiaji kuhamishiana uniti za vifurushi pamoja na mtoa huduma kumwezesha mtumiaji kununua uniti za kifurushi pindi kifurushi chake kinapokaribia kuisha,” alieleza.
Katika suala la bando kuisha kabla ya muda wake, alisema simu za sauti mtumia huduma akipiga, anapewa taarifa ya kiasi gani alichotumia na anaweza kulinganisha kiwango alichotumia kwa kuangalia salio na kupata ujumbe mfupi.