Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania ya 1 Afrika umeme nchi yote

De156a7d17b5da1c07d998e0fe22a14d Tanzania ya 1 Afrika umeme nchi yote

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme nchini kote kwa asilimia 80.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kwenye mkutano wa viongozi wa dini kutoka kamati za amani za mikoa Tanzania bara na Zanzibar.

"Leo hii Tanzania ni ya kwanza barani Afrika kwa kusambaza umeme kote nchini hadi vijijini na kufikisha asilimia 80. Kuna nchi ngapi barani Afrika, lakini Tanzania imefanikiwa kuwa ya kwanza. Tumeweza kufikia vijiji 9,112 Tanzania na hadi Aprili 2020 na tumetumia shilingi trilioni 2.27," alisema Majaliwa.

Mkutano huo uliandaliwa kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano katika ustawi wa amani, uzalendo na kumtanguliza Mungu.

Majaliwa alisema, ushirikiano mkubwa wanauonesha viongozi wa dini kwa Serikali, umewezesha kufanyika mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za upatikanaji wa nishati kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.

Mbali ya upatikanaji wa umeme nchini, Waziri Mkuu alieleza mambo mengine 15 yaliyofanyika kwa ufanisi chini ya uongozi wa Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kurejesha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma; mapambano dhidi ya dawa za kulevya; ulinzi wa rasilimali za taifa; kuimarika kwa ukusanyaji mapato na kukua kwa uchumi.

"Tunao uwezo wa kuhimili ujenzi wa viwanda vipya na nipende kuwahakikishia wenye mitaji kwamba Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza. Tulianza na mazao matano ya kimkakati lakini sasa tumeyaongeza. Kupitia kilimo tunazalisha mazao ambayo ni malighafi kwa viwanda vyetu," alisema Majaliwa.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni mapambano dhidi ya umasikini na ukosefu wa ajira; ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya afya; maboresho ya elimu; huduma za maji; ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere, ujenzi wa mradi wa reli kwa kiwango cha kimataifa (SGR); usafiri wa anga; ujenzi wa meli na bandari na ujenzi wa barabara na madaraja.

"Suala la ajira ni kilio cha wote lakini kila nchi inatumia njia yake kukabliana nayo. Je tusingekuwa na miradi ya kimkakati kama SGR na Stieglers' Gorge, hawa watu milioni sita na zaidi wangekuwa wapi kwa sasa?"alihoji Waziri Mkuu.

Alisema, kupitia sekta za viwanda, kilimo, biashara, madini, utalii, miundombinu ya kimkakati na mifumo ya mikopo nafuu, Serikali imezalisha ajira za kutosha kwa Watanzania.

"Kupitia ujenzi wa viwanda vipya,tumetengeneza jumla ya ajira zipatazo 482,601 na kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya SGR, Stieglers' Gorge, ujenzi wa shule, hospitali na ufufuaji wa mashirika yetu tumefanikiwa kutengeneza ajira zipatazo 6,032,299."

Mapema,akitoa wasilisho la viongozi wa dini, Katibu wa Kamati ya Amani, Askofu Jackson Sosthenes alisema lengo la mkutano huo ni kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua iliyofikiwa ya kuwa na uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema ujasiri wa Rais Magufuli wa kutozuia ibada na kukataa kufungia watu ndani ulimpendeza Mwenyezi Mungu na akaamua kuifanya Tanzania kuwa nyota inayong'ara ulimwenguni.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry ambaye alikuwa wa kwanza kutoa salamu za viongozi wakuu wa dini, alisema mtu mwenye akili anahitaji pointi ndogo tu kuona kinachofanywa na Rais Magufuli.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa alisema amani ni msingi wa maendeleo yote.

"Viashiria vya ukosefu wa amani hatuvipendi, na tunaviombea vitoweke katika jina la Mungu…sisi viongozi wa dini tutaendelea kuiombea nchi yetu. Mungu anaipenda sana Tanzania, na hata tulipopita kwenye bonde la uvuli wa mauti la COVID 19, bado alituvusha. Tuendelee kumheshimu Mungu, kumtii na tuendelee kumwabudu Mungu," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Nooman Jongo alisema zamani Tanzania iliathiriwa mambo matatu ya udini, ukabila na uchama lakini kwa sasa hayapo.

Askofu Michael Hafidhi wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar aliwataka viongozi wa vyama vya siasa waache kuwasema wenzao vibaya na kutumia majina ya maaskofu na sheikh kwa manufaa yao.

Chanzo: habarileo.co.tz