Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuongeza uwekezaji Kenya

8003b35147f01c92557f7318bd1b47d3.png Tanzania kuongeza uwekezaji Kenya

Wed, 5 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan amemuahidi Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuwa Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na imejipanga kuwekeza nchini humo ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi.

Marais hao jana walizungumza namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizo hasa vinavyotokea mipakani na walisaini mikataba miwili ukiwemo ya bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa na nishati ya umeme na gesi.

Kibiashara, katika kipindi cha miaka mitano wastani wa biashara ya thamani ya Sh trilioni moja za Kitanzania ilifanyika na hadi sasa kampuni zaidi ya 500 za Kenya zimewekeza nchini Tanzania.

Rais Samia jana alimuahidi Rais Kenyatta kuwa, Tanzania imejipanga kuingia nchini humo kwa nguvu zote hivi sasa.

Aliyasema hayo alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Nairobi.

Rais Samia yupo Kenya kwa ziara ya siku mbili. Aprili 11 alikwenda Uganda kushuhudia kusainiwa kwa mkataba ya bomba la mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

“Tumezungumza na Rais Kenyatta na tumejadili mambo mengi kama alivyosema Rais Kenyatta katika kukuza uhusiano baina ya nchi zetu mbili. Tanzania na Kenya si tu majirani bali ni ujirani wa kindugu, ameniambia mpaka wa Tanzania na Kenya ndio mkubwa zaidi katika mipaka ya nchi hiyo na wananchi wanaoishi mipakani ni ndugu.

“Kutokana na urafiki tulionao tumeweza kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa mfano wakati wa mazungumzo yetu tumemuarifu kaka yangu rais Kenyatta kuwa, Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji ndani ya nchi ya Tanzania ikitanguliwa na mataifa mengi lakini kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ya kwanza na ulimwengu inashika nafasi ya tano,” alisema Samia.

Alisema Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni

1.7 ambayo imetoa ajira zipatazo 51,000 kwa Watanzania.

Alisema zipo kampuni 30 za Kitanzania ambazo zimewekeza mtaji nchini Kenya wenye thamani ya shilingi za Kenya bilioni

19.330 iliyotoa ajira kwa watu 2,640.

“Lakini nimeweka ahadi kwamba, Tanzania sasa tutakuja kwa nguvu zote Kenya kuja kuwekeza ili kukuza ujazo wa biashara. Lakini mbali na uwekezaji nchi zetu mbili ni wadau wakubwa wa biashara ambapo kwenye miaka mitano iliyopita, wastani wa biashara kati ya Tanzania na Kenya ni Sh trilioni moja za Kitanzania (sawa na Dola milioni 450) bado si kubwa tumeweka ahadi kuikuza, alisema Samia.

Rais Samia alisema walikubaliana namna ya kukuza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo hasa kutokana na fursa nyingi zilizopo.

Alisema walikubaliana kuendelea kushughulikia baadhi ya changamoto hususani vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vinatokea katika mipaka.

“Lakini jingine aliloliongeza Mheshimiwa Rais nakubaliana nalo ni kwa mawaziri wetu wa afya kukaa na kuangalia namna ya kurahisisha mfumo wa kuingia na kuchekiwa kwenye mambo haya ya Covid-19 au corona, watu wetu wapate

huduma za haraka, kupima, kuchekiwa ili waweze kupita na baishara ziendelee,” alisema Samia.

Samia alisema pia walijadiliana na Rais Kenyatta pia kuhusu namna ya kutekeleza miradi ya kimkakati inayohusu usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa na jinsi ya kupata nishati umeme au gesi kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

“Tuna hiyo miradi, mmoja tulishasaini mkataba leo tunachokwenda kufanya ni kusimamia utekelezaji. Lakini pia kuna mmoja unaendelea na mazungumzo yapo karibia kukamilika, nitumie lugha ya Mheshimiwa Rais tutaweka kidole hivi karibuni na mwingine tupo kwenye mazungumzo kuumaliza,” alisema.

Rais Samia alisema wamezungumzia pia suala la bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, mradi wa muda mrefu ambao jana walisaini na kilichobaki ni utekelezaji wake.

Kwa mujibu wa Samia, maeneo mengine waliojadiliana ni mahusiano ya kimataifa hususani namna ya kuimarisha Jumuiya

ya Afrika Mashariki na kuzihimiza nchi wanachama kulipa michango yao ili kuiwezesha jumuiya hiyo kusimama vizuri.

Kenyatta ampongeza Samia Rais Kenyatta alimpongeza Rais Samia na kueleza kuwa ziara yake ni ya kihistoria kwa kuwa amekwenda nchini humo kama Rais wa nchi na mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika Afrika Mashariki.

Kenyatta ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, katika mazungumzo yake na Rais Samia jana, walizungumzia mambo yanayohusu nchi hizo mbili si tu kwa kuwa ni majirani lakini wenye ujirani wa utamaduni wa pamoja (lugha, urithi, ubinadamu na utu tangu enzi za babu zao).

“Tanzania ni nchi ndugu, nilipomkaribisha nilimwambia karibu nyumbani sababu hapa ni nyumbani. Tumepata nafasi ya kuongea mambo mbalimbali, tutaboresha ushirikiano wetu, tumekubaliana mawaziri wakutane mara kwa mara watatue shida ndogo ndogo zinazosumbua watu wetu wakati wanatembeleana na

kuwekeza katika nchi zetu,” alisema Kenyatta.

Alisema nchi hizo zinapaswa kuhakikisha mambo ya kibiashara yamerahisishwa na kuimarisha utamaduni ili kujenga taifa la Kenya na Tanzania. Alisema pia wamekubaliana kuimarisha masuala ya mawasiliano kama reli, ndege, bahari, kanda ya ziwa na barabara.

Kenyatta alisema wamezungumza umuhimu wa kuharakisha barabara ya Malindi, Lungalunga mpaka Bagamoyo na kuanza tena safari za Ziwa Victoria kutoka Jinga, Kisumu nchini Kenya hadi Mwanza na Kigoma, nchini Tanzania ili kurahisisha mwenendo wa usafiri kwa raia wetu na kurahisisha biashara.

Kwa mujibu wa Kenyatta, viongozi hao pia walizungumzia masuala ya usalama wa nchi hizo na wananchi hasa katika kupambana na ugaidi na kuweka mikataba ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam mpaka Mombasa kupata unafuu wa gesi katika taifa la Kenya. Pia wamejadili mikataba kuhusu utalii na mingine mingi.

“Tupo na furaha tele siku ya leo, sababu wewe tunakuona kama dada yetu na ndugu yetu, Tanzania na Kenya ni kitu kimoja na safari hii tutaenda mbali sana kuhakikisha uhusiano wa nchi hizi unaimarika zaidi na zaidi. Hivi karibuni nitatimiza mwaliko wako wa kukaribia nchi ya Tanzania,” alisema.

Oktoba mwaka 2016 aliyekuwa rais wa Tanzania, Dk John Magufuli alitembelea Kenya na kukutana na mwenyeji wake Uhuru Kenyatta. Katika ziara hiyo, nchi hizo zilikubaliana kushirikiana katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ikiwamo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo nchini Tanzania hadi Malindi nchini Kenya.

Mapokezi ya Samia nchini humo Rais Samia aliwasili jana katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta saa 9:45 asubuhi kwa ndege ya Tanzania aina ya Airbus A 220-300 na kupokelewa na baadhi ya viongozi wa serikali hiyo Katika kiwanja hicho, alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Raychelle Omamo na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa nchi hiyo, Amina Mohamed.

Baada ya kuwasili, msafara wa Rais Samia ulielekea katika hoteli ya Serena. Katika baadhi ya maeneo, wananchi walionekana wamesimama kando ya barabara kwa mapokezi ya Rais Samia wakati akielekea Ikulu jijini Nairobi alikopokelewa na mwenyeji wake, Rais Kenyatta.

Nyimbo za Taifa za nchi hizo mbili zilipigwa katika viwanja vya Ikulu, jijini Nairobi pamoja wimbo wa Afrika Mashariki na kisha Rais Samia alipigiwa mizinga 21 ya heshima ya kijeshi kama rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania.

Rais Samia alikagua gwaride na kisha kufanya mazungumzo na Rais Kenyatta kuhusu uhusiano baina ya mataifa hayo mawili na namna ya kuuimarisha zaidi ya sasa kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Leo Rais Samia anatarajiwa kuhutubia Bunge la pamoja la nchi hiyo. Pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania na jumuiya ya wafanyabiashara wanawake, jijini Nairobi.

Raia Samia pia alisema katika sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania mwaka huu, amemwalika kwa Rais Kenyatta awe mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz