Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuimarisha biashara, uwekezaji EAC

C0174b11a248cd811a9821bfb8d9ba8f Tanzania kuimarisha biashara, uwekezaji EAC

Tue, 20 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BIASHARA na uwekezaji katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itaongezeka kwa kiwango kikubwa baada ya miradi mikubwa ya ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika inayotekelezwa na Tanzania kukamilika.

Aidha, baada ya kukamilika miradi mikubwa ya ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria, ambazo ni MV Mwanza Hapa Kazi Tu, MV Victoria, MV Butiama, MV Umoja na MV Clarias, serikali imeelekeza juhudi zake kukamilisha miradi ya ujenzi wa meli na kukarabati nyingine katika Ziwa Tanganyika.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho wakati akizungumza na HabariLEO kuhusu mchakato wa kununua meli mbili za abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika ikiwa ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu.

Alisema kukamilika kwa kazi hiyo kutafungua milango kwa nchi za Afrika Mashariki kuwekeza katika usafiri wa majini na kufanya biashara baina ya mataifa yote ya Afrika Mashariki, huku Tanzania ikinufaika zaidi na fursa hizo.

“Katika Ziwa Victoria mataifa yatakayofanya biashara na uwekezaji wa majini ni Tanzania, Kenya na Uganda, wakati katika Ziwa Tanganyika ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda,” alisema.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Marine Services Company LTD, Erick Hamissi aliliambia gazeti hili kuwa, baada ya utaratibu wa kutangaza tenda kukamilika, hatua iliyobaki ni kwa mshindi wa zabuni kupewa barua ya ushindi kufuatana na sheria za manunuzi zinavyotaka.

Alisema mchakato wa kutafuta zabuni ya ujenzi wa meli hiyo umefikia hatua za mwisho na muda wowote ndani ya mwezi huu mshindi wa zabuni atakabidhiwa barua ya ushindi ili kuanza kazi mara moja ya ujenzi wa meli mbili, moja ya abiria na nyingine ya mizigo.

Hamissi ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, alisema meli ya abiria itakuwa na uwezo wa kubeba watu 1,200 na mizigo tani 400 na itafanya safari zake kati ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kama vile Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa upande wa meli ya mizigo, alisema itakuwa na uwezo wa kubeba tani 4,000 na itabeba mizigo ya nchi nne za Afrika Mashariki, Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika ahadi aliyoitoa mwaka jana, Magufuli alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali mbali na kununua meli mpya mbili, imetenga Sh bilioni 10 kukarabati meli ya MV Liemba na MV Sangara iliyotengewa Sh bilioni sita.

Chanzo: www.habarileo.co.tz