Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania ina uthubutu wa kipekee  katika  maendeleo-AfDB

7f855ac8497774f5ef4c407a638baebf Tanzania ina uthubutu wa kipekee katika maendeleo-AfDB

Sun, 29 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipongeza Serikali kwa kupiga hatua mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi ikisema Tanzania ina uthubutu wa kipekee linapokuja suala la maendeleo.

Aliyekuwa Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo nchini, Dk Alex Mubiru ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi katika ofisi ya Rais wa benki hiyo alisema hayo juzi katika hafla ya kumuaga iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa niaba ya AfDB, Mubiru aliahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hususani katika masuala ya miundombinu ya barabara na umeme.

Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, iliipongeza AfDB kwa kuendeleza ushirikiano wao wa muda mrefu katika kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

“Dk Mubiru kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika umesaidia kusukuma fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati hapa nchini na katika miaka miwili uliyokaa hapa, Tanzania imeweza kunufaika na fedha za kutekeleza miradi yenye thamani ya takribani dola bilioni 2.5”, alisema Waziri Mpango.

Alisema miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na benki hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu jijini Dodoma ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma na kituo kikubwa cha umeme cha Zuzu.

Mpango alisema miradi mingine ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 260 kutoka Manyovu, Buhingwe, Kasulu hadi Kabingu mkoani Kigoma pamoja na mradi wa kuunganisha mkoa huo na umeme wa gridi kuu ya Taifa.

“Vile vile hivi punde Benki ya Maendeleo ya Afrika imeridhia kutoa dola milioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa kubwa la umeme kutoka mto Malagalasi ambao unatarajiwa kuzalisha takribani megawati 45 za umeme kwa ajili ya Mkoa wa kigoma”, alisema.

Waziri Mpango alimuomba Mubiru kufikisha salamu za Serikali ya Tanzania na watanzania kwa ujumla kwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kubainisha kuwa anaamini Mwakilishi Mkazi atakayeteuliwa atakuja kuendeleza walipoishia.

Chanzo: habarileo.co.tz