Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Rwanda kuendeleza ushirikiano na kukuza mahusiano

Ed87361d3d8912e1fc3b55157827a35a.jpeg Tanzania, Rwanda kuendeleza ushirikiano na kukuza mahusiano

Thu, 3 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia Suluhu Hassan mapema leo amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame uliowasilishwa na Mjumbe Maalum na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda, Dk Vincent Biruta.

Katika taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema Rais Kagame ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk John Pombe Magufuli na amempongeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais na amemhakikishia kuwa Rwanda ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.

Rais Kagame amesema hali ya Rwanda ni shwari, inaendelea kusukuma mbele maendeleo yake na ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani katika utekelezaji wa miradi ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) ya kuunganisha Jiji la Kigali (Rwanda) na Isaka (Tanzania) ambayo itasaidia usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Rwanda.

Rais Samia amemshukuru Rais Kagame kwa kumtumia ujumbe huo uliojumuisha salamu za pole na pongezi na amemhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Rwanda.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya pamoja, ametaka Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Tanzania na Rwanda (JPC) ikutane ili kuongeza msukumo katika miradi hiyo pamoja na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Maeneo mengine ambayo ametaka JPC ifanyie kazi ni kuimarisha usafirishaji wa minofu ya samaki kutoka Mwanza kupitia Shirika la Ndege la Rwanda na kuharakisha ujenzi wa bandari kavu ya Isaka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz