Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Kenya zazungumza mahindi kuzuiwa mpakani

958d9e7abf8c2dcee68409581e237817.png Tanzania, Kenya zazungumza mahindi kuzuiwa mpakani

Wed, 10 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi (pichani) amesema serikali za Tanzania na Kenya zinaendelea kuzungumza kumaliza mzozo kuhusu mahindi yanayozuiwa kuingizwa nchini humo.

Dk Abbasi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa jijini hapa jana kuwa ni kweli kuna magari ya Tanzania yamezuiwa kwenya mpaka wa Namanga mkoani Arusha, lakini kwenye mipaka ya Horohoro, Tanga na mipaka mingine yanapita.

“Katika hali kama hiyo sisi serikali kwa serikali lazima tuzungumze na mazungumzo yanaendelea kwa nini Horohoro yanapita lakini Namanga yamezuiliwa kwa hiyo ni suala ambalo linafanyiwa kazi,” alisema Dk Abbasi.

Jana Chama Cha ACT Wazalendo kilisema mahindi ya Tanzania ni salama hivyo serikali izungumze na Serikali ya Kenya kumaliza mzozo kuhusu soko la zao hilo. Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto alisema jana kuwa Watanzania hawalimi mahindi yenye sumu na kwamba wanakula mazao hayo hayo yanayouzwa Kenya.

Taarifa ya Idara ya Habari na Uenezi, ACT Wazalendo ilieleza kuwa Zitto alisema mzozo kuhusu soko la mahindi na jambo la kidiplomasia kuhusu biashara na si sumu.

“Kwenye hili la mahindi ninaamini kuwa hoja sio aflatoxin (sumukuvu). Nchi zetu zimekuwa zikifanya juhudi za pamoja kukabiliana na aflatoxin na ushahidi ni sheria pendekezwa EAC.

Hili ni jambo la diplomasia.

Tanzania na Kenya wakae wazungumze.

“Kuna taratibu za kisheria za kufuata kukagua Ubora wa mahindi. Zifuatwe hizo,” alisema Zitto.

Taarifa hiyo kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho ilieleza kuwa mahindi ya Tanzania ni salama na yana kiwango cha aflatoxins kinachokubalika na kwamba Kenya na Tanzania wamekuwa wakichukua hatua kukabiliana na aflatoxins kupitia EAC na kuna muswada wa sheria ya EALA kuhusu hilo.

“Aflatoxin imetumika kama sababu tu lakini sio hoja. Hoja ni biashara”alisema Zitto.

Alisema amri ya kuzuia mahindi ya Tanzania kuingia Kenya haistahili kuwa juu ya mkataba wa EAC na Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na kila mwanachama wa EAC lazima aheshimu mkataba na itifaki.

Wakati huohuo, Mwandishi Wetu, Amina Omari anaripoti kutoka Mkinga kuwa uongozi wa Mkoa wa Tanga umekanusha taarifa zilizodai mahindi yanayoingizwa Kenya kutoka Tanzania hayana viwango vya ubora kwa matumizi ya binadamu.

Mkuu wa mkoa huo, Martine Shigela alitoa msimamo huo alipofanya ziara katika mpaka wa Horohoro na kusema wanaoeneza taarifa hizo wana nia mbaya ya kuvuruga uhusiano mzuri wa kibiashara kati ya nchi hizo.

Shigela alisema mpaka huo una wataalamu wa usalama wa bidhaa za chakula hivyo hakuna uwezekano wa kupitisha bidhaa zisizo na ubora. “Tunataka muendelee na biashara kusafirisha mahindi kama kawaida, taarifa ya kwamba mahindi yanayotoka Tanzania hayafai kuliwa na watu wa Kenya kwa sababu hayana ubora sio za kweli.

Taarifa ni kwamba kila siku mahindi yanapitishwa na kuvuka mpaka kupelekwa Kenya bila kizuizi chochote,” alisema Shigela.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwisho wa wiki jumla tani 510 za mahindi zilipitishiwa mpakani Horohoro kwenda Kenya hivyo kama yangekuwa na kasoro yangebainika na kuzuiwa.

Aliwataka wafanyabiashara na wananchi katika eneo hilo waendelee kufanya biashara kwa kuwa serikali ina mpango wa kuziboresha ili zifanyike saa 24.

Mfanyabiashara wa Kenya, Jafo Otara ambaye amekuwa akisafirisha mahindi kutoka Tanzania kwa zaidi ya miaka sita, alisema tayari wamewasiliana na mwanasheria nchini kwao ili kumfungulia mashitaka aliyehusika kusambaza taarifa za uongo.

“Tumezungumza na Waziri wa Kilimo na Chakula wa nchini kwetu na amekana kuwepo kwa taarifa hiyo na kusema hiyo taarifa itakuwa imetoka msituni na sio ya kwake, na kuwa kesho Jumatatu (jana) tarehe 8 Machi 2021, anakwenda kutoa taarifa kwa waandishi wa habari,” alisema Otara.

Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha Horohoro, Nsajigwa Mwambegele alisema mwaka jana tani 72,000 za bidhaa zilipitishwa kwenye mpaka huo kutoka Kenya zikiwa na thamani ya Sh bilioni 98.

Alisema tani 53,000 za bidhaa kutoka Tanzania zilipitishwa mpakani hapo kwenda Kenya zikiwa na thamani ya Sh bilioni 50. “Mpaka huu ni wa kimkakati hivyo ni jukumu. letu kuhakikisha tunaboreshs mahusiano mazuri kwa ajili ya maendeleo ya pande zote kiuchumi na kijamii,” alisema Mbwambegele.

Chanzo: www.habarileo.co.tz