Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, China kunufaika biashara mtandaoni

C713afd83f8e9ac91a907ec170dbe51b.jpeg Tanzania, China kunufaika biashara mtandaoni

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkutano wa nne wa awamu ya 13 ya Bunge la Umma la China umefunguliwa leo hapa Beijing, ukiwa na ajenda tatu kuu ambazo ni kusikiliza na kujadili ripoti ya kazi za serikali, kujadili mpango wa 14 wa maendeleo ya miaka mitano, na mwongozo wa malengo ya mwaka 2035.

Hotuba kuhusu utendaji wa serikali kimsingi inaangalia mambo mawili.

Kwanza ni utendaji wa serikali katika utekelezaji wa mipango ya mwaka uliotangulia, ambapo Waziri mkuu amezungumzia mafanikio iliyopata China katika kutokomeza umaskini katika mazingira magumu ya uchumi na janga na COVID-19, na pili ni mikakati na mipango kwa ajili ya maendeleo kwa mwaka huu na miaka ijayo, hasa mpango wa 14 wa maendeleo ya miaka mitano.

Kutokana na ukubwa na uchumi wa China na jinsi uchumi wa China ulivyofungamana na uchumi wa nchi mbalimbali duniani, karibu dunia nzima inafuatilia ripoti ya waziri mkuu Li, ili kujua mipango ya China kwa mwaka huu itakuwa na maana gani kwa nchi zao, na hata kwa uchumi wa dunia kwa ujumla.

Moja ya mambo aliyotaja Waziri mkuu kwenye ripoti yake ni kuhusu China kuendeleza uchumi wa kidigitali.

Waziri mkuu amesema China itaendeleza uchumi wa kidigitali na kuufanya uwe wa kisasa zaidi na kutoa fursa zaidi kwa watu mbalimbali duniani. Hatua hii inakuja katika kipindi ambacho janga la COVID-19 limeleta changamooto mbalimbali kwenye sekta ya biashara, na kufanya iwe vigumu kwa wafanyabiasha kuagiza na kusafirisha bidhaa zao kwenye soko la China.

Alichokisema Waziri Mkuu Li tayari kimeanza kutekelezwa na kuna mifano kadhaa ambayo baadhi ya balozi za nchi za Afrika nchini China, zilitumia mtandao wa internet kutangaza bidhaa kwenye soko la China, Tanzania ikiwa ni moja wapo.

Balozi wa Tanzania nchini China Bw. Mbelwa Kairuki amepongeza hotuba ya waziri mkuu Li, na kusema kuwa tayari Tanzania imeanza kushirikiana na China kwenye maswala ya biashara mtandao, makampuni mbalimbali ya China kama Alibaba (inayopanga kuanza kuuza mabondo ya samaki na kahawa) na Jingdong kutangaza na kuuza bidhaa za Tanzania kwenye soko la China.

Lakini pia amesema kuna miradi mingi ya mambo ya kidigitali nchini Tanzania inayohitaji uwekezaji kutoka China.

Hivi karibuni Rais Xi Jinping wa China alisema, “Uchumi wa kidigitali ni mwelekeo wa maendeleo ya siku za baadaye ya dunia” na alitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu usimamizi wa kidigitali wa dunia na maendeleo ya uchumi wa kidigitali duniani. Kinachofanywa kati ya Tanzania na makampuni ya kidigitali ya China, kinaendana na mapendekezo hayo ya Rais Xi.

Waziri mkuu pia amezungumzia kuhusu China kuendelea kufungua zaidi soko lake kwa dunia, na kuhimiza kujenga kwa pamoja maendeleo ya sifa ya juu ya “Ukanda Mmoja na Njia Moja”, kuzindua mtandao wa eneo la bishara huria wa kiwango cha juu linalofunguliwa kwa dunia nzima.

Balozi Kairuki amesema kutekeleza vizuri pendekezo la “ukanda mmoja, njia moja” ni fursa nzuri kwa nchi mbalimbali kwenye maswala ya uwekezaji, na hasa kwenye wa miundo mbinu.

Amesema China na Tanzania tayari zinashirikiana na zinatarajia kushirikiana zaidi kwenye eneo la ujenzi wa miundo mbinu.

Ametoa mfano wa mradi uliokamilika wa daraja la Kijazi Ubungo Dar es salaam, upanuzi wa banadari ya Dar es salaam, ujendi wa daraja mkoani Kigoma, na pia mradi unaokaribia kuanza mwisho mwa mwaka huu wa kipande cha reli ya kati.

Mkutano huu utaendelea hadi tarehe 11. Katik kipindi hiki wachambuzi wa maswala ya kiuchumi na maswala ya kidiplomasia, watafuatilia kwa undani yaliyomo kwenye ripoti nzima ya Waziri Mkuu Li, na kufuatilia mipango ya utekelezaji wake katika siku zijazo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz