Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Burundi zasaini ushirikiano wa kidiplomasia

68e44bcfd68bc6bb2663efcc48b56b79 Tanzania, Burundi zasaini ushirikiano wa kidiplomasia

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TANZANIA na Burundi zimetiliana saini makubaliano katika ushirikiano wa masuala mbalimbali ikiwamo diplomasia, biashara na uwekezaji, ulinzi, usalama na uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi inayounganisha nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema ushirikiano uliopo na nchi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wa pande zote na Tanzania haitakubali kuona ushirikiano ukivunjika.

Profesa Kabudi alisema hayo akifungua mkutano wa sita wa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) kati ya nchi hizo. Alisema kusainiwa kwa makubaliano ya pamoja kunalenga kuimarisha uhusiano katika kuweka mikakati ya pamoja ya kimaendeleo.

Katika mkutano huo, nchi hizo zilitiliana saini makubaliano hayo katika ushirikiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji, ulinzi na usalama, uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi inayounganisha nchi hizo mbili na masuala ya kijamii yanayogusa moja kwa moja wananchi wa nchi hizo.

Kabudi alisema kuwa msimamo wa Rais John Magufuli na Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimiye katika kuweka mikakati ya kukuza uchumi na maendeleo kwa ajili ya wananchi wao, ndio unaoufanya ushirikiano huo kuwa muhimu na wa kindugu.

Alitaja moja ya miradi ambayo inaifanya Tanzania na Burundi kudumisha ushirikiano huo ni mradi wa reli kutoka Uvinza mkoani Kigoma kwenda Kabanga Msongati nchini Burundi, ambako kuna machimbo ya madini ya nickel.

“Pamoja na mkutano huu Tanzania itapigana bega kwa bega kuona Burundi inashirikishwa na kukubaliwa kuwa mwanachama wa SADC, jambo ambalo litawezesha mikakati na mipango yetu kwenda vizuri na kwa haraka,”alisema Profesa Kabudi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Maendeleo wa Burundi, Balozi Albert Shingiro alisema kwa sasa Burundi ina amani na hivyo mkakati mkubwa wa Rais wao, Ndayishimiye ni kukuza ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na washirika wake ikiwamo Tanzania.

“Kwa sasa muda wa kumiliki rasilimali zetu umefika na ushirikiano huu baina ya Burundi na Tanzania ni kwa manufaa ya nchi hizi mbili,”alisema Balozi Shingiro.

Akiwakaribisha viongozi na wageni waliohudhuria mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa mkoa wake unapiga hatua kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz