Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Burundi zasaini makubaliano ya usafiri EAC

808d37c4d8ed69d3eff5d2bac0f82475 Tanzania, Burundi zasaini makubaliano ya usafiri EAC

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA na Burundi zimetia saini makubaliano ya uwezeshaji wa usafi ri wa ukanda wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ukilenga kuharakisha na kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka Tanzania hadi Bujumbura nchini Burundi.

Pia kuboresha Kituo cha Pamoja cha Forodha katika mpaka wa Tanzania na Burundi kilichopo Manyovu wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Manyovu wilayani Buhigwe jana kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Elius Mwakalinga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mitambo na Makazi ya Jamii wa Burundi, Egide Nijimbele.

Pia alikuwepo Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Steven Mlote na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uwezeshaji wa Usafiri wa Ukanda wa Kati (CCTTFA), Dieudonne Dukundane.

Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa makubalianio hayo, Mwakalinga alisema utekelezaji wa makubaliano hayo utaleta matokeo chanya kwa serikali na wananchi wa nchi hizo mbili katika kukuza uchumi wa nchi huku kukiwa na lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja likitiliwa mkazo katika utekelezaji wake.

Mwakalinga alisema kuimarishwa kwa usafiri na usafirishaji katika nchi hizo mbili, utaharakisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Aliahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo kwa Tanzania unatekelezwa na kukamilika kwa wakati.

“Pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami, pia mpango utahusisha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha katika mpaka wa Tanzania na Burundi eneo la Manyovu mkoani Kigoma na ujenzi wa kituo kama hicho eneo la Mugina Mkoa wa Makamba nchini Burundi,” alisema Mwakalinga.

Alieleza kuwa kwa sasa Tanzania inatekeleza ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye kilometa 261 kutoka Kabingo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma hadi Manyovu, na wakandarasi wako maeneo ya utekelezaji wa mradi huku kukianza ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu.

Ujumbe wa nchi hizo mbili, ulitembelea eneo litakalojengwa Kituo cha Forodha Manyovu na Mugina nchini Burundi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mitambo na Makazi ya Jamii wa Burundi, Egide Nijimbele alisema Burundi ipo katika utekelezaji wa barabara ya kiwango cha lami kutoka mpaka wa Manyovu nchini Tanzania kwenda Bujumbura nchini Burundi ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na shehena.

Katibu Mkuu Msaidizi wa EAC, Mlote alisema makubaliano hayo yanaenda sambamba na kukabidhi eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu, ambacho kitaongeza tija katika biashara na kiuchumi EAC.

Katibu Mtendaji wa CCTTFA, Dieudonne Dukundane alisema njia ya kutoka bandari ya Dar es Salaam kupitia mpaka wa Manyovu ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi ya EAC, kwani pia ni muhimu kwa usafirishaji wa abiria na shehena kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Alisema wafanyabiashara wamekuwa na malalamiko mengi ya kutumia muda mwingi kusafirisha shehena kupitia mpaka wa Kabanga nchini Tanzania kutokea Kobero nchini Burundi, hivyo kuimarishwa kwa ujenzi wa kituo cha forodha Manyovu ni ukombozi mkubwa kwa wafanyabiashara.

Chanzo: habarileo.co.tz