Kampuni moja ya Ufaransa inajitahidi kuondoa takriban tani milioni 20 za taka za sumu zenye mionzi ambazo zilisalia kufuatia kufungwa kwa shughuli zake katika migodi mikubwa ya madini ya uranium katika eneo la Arlit kaskazini mwa Niger.
Kampuni kubwa ya nyuklia ya Ufaransa, Areva, ambayo ilibadilisha jina lake kuwa Orano, ilifanya kazi katika eneo la jangwa chini ya kampuni tanzu inayoitwa Akouta Mining Company (COMINAK) kutoka 1978 kabla ya kusitisha shughuli zake mnamo 2021. Mahaman Sani Abdoulaye, mkurugenzi mkuu wa COMINAK, aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Niger Niamey Alhamisi kwamba zoezi la kuondoa taka hizo katika eneo husika litachukua miaka 10.
Mradi huo wa kuondoa taka hizo unakadiriwa kugharimu dola milioni 160 na unatarajiwa kukabiliana na uchafu huo na kuzuia maafa ya kiafya na kimazingira ambayo yamezua hofu miongoni mwa wakazi wa eneo jirani.
Hifadhi za urani katika eneo hilo zilikwisha baada ya tani 75,000 za urani kuchimbwa. Aghalabu ya urani hiyo ilitumika katika vinu vya nyuklia vya kusambaza umeme Ufaransa.
Ripoti zinaonyesha kuwa uchafu huo wa urani umezua hofu kubwa kwa wakazi wapatao 200,000 wa mji wa Arlit na maeneo jirani.
Wasiwasi mkubwa ni vifuniko vilivyo juu ya mapipa ya taka za nyuklia chini ya ardhi kwani vinaweza kupata nyufa na kuachilia gesi za sumu zinazosababisha saratani sambamba na kuharibu vyanzo vya maji safi katika eneo hilo.
Rhamar Ilatoufegh, mkuu wa Aghir in Man, NGO ya haki za binadamu na ulinzi wa mazingira huko Arlit, alisema taka hizo za sumu zilizoachwa na shirika hilo la Ufaransa" ni "urithi mbaya zaidi ambao uchimbaji wa uranium uliacha kwa wakazi."
Meya wa Arlit Abdourahmane Maouli pia alikiri tatizo la sumu ya uranium.
Niger ni mojawapo ya vyanzo vikubwa zaidi vya urani duniani lakini nchi hiyo ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani huku madini yake ya urani yakiwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Ufaransa.