Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tani 216 mahindi zazuiwa mpakani Holili

A39420f3360c272c7ef6c85e03b52d76 Tani 216 mahindi zazuiwa mpakani Holili

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHEHENA ya mahindi tani 216 yamezuiwa katika mpaka wa Holili upande wa Kenya yakisubiri majibu ya vipimo vya sampuli zilizochukuliwa na mamlaka za nchi hiyo.

Meneja wa Forodha Mkoa wa Kilimanjaro, Edwin Iwato aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mpakani hapo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Iwato alisema mahindi hayo yaliyokuwa kwenye magari 15 yalizuiwa Machi 5, mwaka huu na mpaka sasa wanasubiri majibu ya sampuli zilizochukuliwa.

Alisema tangu Machi 5 hadi 8 kumekuwa na changamoto ya biashara ya mahindi katika mpaka huo. “Shehena ya mahindi tani 216 kutoka kwa wakulima wa Tanzania yamekwama upande wa Kenya kusubiri taratibu za majibu ya vipimo. Tunasubria tujue hatma ya mahindi hayo ambayo yapo kwenye magari 15 ya mizigo,” alisema Iwato.

Aliongeza, “Tunasubiri wenzetu wa Kenya wakamilishe utaratibu huo na ni changamoto ambayo imejitokeza na imeathiri kidogo mzunguko wa biashara hiyo ya mahindi hapa mpakani.”

Iwato alisema, serikali inaendelea kushughulikia suala hilo ili kuweza kukwamua mkwamo huo na kuwezesha biashara kwa pande zote kuendelea kama kawaida.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mahindi katika mpaka wa Holili, walionesha kushangazwa na kauli ya Kenya kudai kuwa mahindi yana sumu wakieleza kuwa wamefanya biashara hiyo zaidi ya miaka 20 bila matatizo.

Zuberi Khamis alisema kauli ya Serikali ya Kenya kwamba mahindi kutoka Tanzania yana sumu si ya kweli.

“Tumekuwa tukishirikiana vizuri na wafanyabiashara wa Kenya na tumefanya biashara ya nafaka kwa muda mrefu bila matatizo lakini leo tunashangaa kusikia mahindi ya Tanzania yanasumu hizo ni hila hamna lolote,” alisema.

Ramadhani Bakari alisema magari yamezuiwa upande wa Kenya na kwamba katika soko la kimataifa la nafaka Holili, kuna shehena kubwa ya mahindi.

“Tunaiomba sana serikali hizi mbili ziweze kukaa kwa pamoja na kuona namna ya kumaliza tatizo hili, maana tumekuwa tukishirikiana vizuri, kwa kuda mrefu na hatujawahi kusikua kuwa watu wamefariki Kenya au Tanzania kutokana na kula nafaka zenye sumu,” alisema Bakari.

Chanzo: www.habarileo.co.tz