Watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa kundi la Allied Democratic Forces wamewaua takriban watu 17 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa ni mauaji ya pili ya umati katika kipindi cha chini ya wiki moja.
Pia walichoma moto majengo wakati wa uvamizi wa alfajiri huko Kirindera katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Siku ya Jumatano, watu 45 waliuawa wakati wa uvamizi wa vijiji viwili vya waasi hao hao - ambao wanasemekana kuwa na uhusiano na kundi la Islamic State.
Mazungumzo ya amani yamejaribiwa, lakini jibu la kimataifa kwa mgogoro wa mashariki mwa DR Congo ni kutuma wanajeshi zaidi.
Jeshi la Uganda limekuwa Kivu Kaskazini kupambana na waasi wa ADF kwa zaidi ya mwaka mmoja lakini bila mafanikio.
Wiki iliyopita pekee ADF iliua makumi ya raia katika vijiji vitatu. Pia kumekuwa na tahadhari kubwa kwa waasi wa M23 ambao wanaripotiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Kigali daima imekanusha shutuma hizo. Angola sasa inatuma wanajeshi Kivu Kaskazini. Wanajeshi wa Kenya na Burundi pia wapo.
Matumaini ni kwamba nchi hizi zimeungana dhidi ya makundi yote ya waasi na hazigeuki kunyonya madini ya DR Congo kama ilivyotokea hapo awali.