Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takriban watu 15 wameuawa katika maporomoko ya udongo DRC

Maporomoko Drc Takriban watu 15 wameuawa katika maporomoko ya udongo nchini DR Congo

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wasiopungua 15 wamefariki katika maporomoko ya udongo katika mji wa Bukavu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mji huo ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, umekumbwa na mvua kubwa ambayo imesababisha maporomoko ya ardhi ambayo yamezika nyumba kadhaa.

Katika wilaya ya Ndedere jijini, chifu wa kitongoji hicho Albert Migabo Nyagaza amewaambia waandishi habari kuwa "baba, watoto wake watano na wajukuu wawili walizikwa hai katika maporomoko ya udongo na nyumba yao kuharibiwa".

Amesema kuwa maporomoko ya ardhi yalitokea mwendo wa saa sita usiku Jumapili. "Tulisikia sauti kubwa kama radi," mkazi wa eneo hilo Medo Igunzi Munene amesema.

Ameongeza kuwa aliona "ukuta wa nyumba ukiporomoka kwenye nyumba nyingine iliyokuwa chini ambapo watu wanane walikuwa wamelala."

Katika wilaya jirani ya Panzi, watu wasiopungua saba wamekufa katika mazingira sawa na hayo. Bukavu imekumbwa na mfululizo wa maporomoko ya ardhi na majengo kuporomoka mwaka huu.

Jiji lenye msongamano mkubwa wa watu katika ufuo wa kusini wa Ziwa Kivu awali liliundwa kwa ajili ya wakazi 100,000. Leo kuna wakazi wapatao milioni mbili, ingawa ukosefu wa sensa hufanya iwe vigumu kuthibitisha idadi sahihi ya watu. Hali baada ya mafuriko Hanang mkoani Manyara nchini Tanzania

Katika nchi jirani ya Tanzania , idadi ya waliofariki kutokana na maafa ya mvua zilizosababisha mafuriko na maporomoko ya matope huko Hanang mkoani Manyara imekaribia watu 76. Maporomoko hayo ya matope yameharibu kaya 1,150 na hivyo kuathiri watu 5,600.

Ijumaa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilitahadharisha kuhusu tishio linaloongezeka kwa usalama wa chakula Afrika Mashariki kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi za ukanda huo.

WFP imeonya kuwa, mafuriko hayo yanarudisha nyuma juhudi changa zinazofanywa na nchi za Afrika Mashariki za kukabiliana na madiliko ya hali ya hewa baada ya baadhi ya nchi kuathiriwa na ukame wa muda mrefu.

Karibu watu milioni 3 wameathiriwa na mafuriko Afrika Mashariki huku zaidi ya milioni 1.2 kati yao wakilazimika kuhama makazi yao baada ya mvua zisizokoma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live