Hali ya taharuk imezuka nchini Liberia baada ya watoto wawili wa Marais wa zamani wanchi hiyo na afisa wa uhamiaji kuuawa hivi karibuni.
Msemaji wa polisi Moses Carter ameithibitishia BBC siku ya Jumatano kuwa mauaji ya watoto wa aliyekuwa rais wa Liberia William R. Tolbert, Jr, yalitokea Jumatatu wiki hii.
Mwili wa Mchungaji William R. Tolbert, III ulikutwa umetapakaa damu kitandani kwake , katika makazi yake yaliyopo kisiwa cha Bushrod, Monrovia.
Baba yake aliuawa kikatili na mwili wake kukatwakatwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Samuel Doe ambayo yalipindua utawala wake wa miaka tisa tarehe 12 Aprili 1980.
Na kama marehemu baba yake, Mchungaji Tolbert alikuwa mhubiri na balozi wa amani wa Liberia.
Kifo chake kimetokea siku moja baada ya mwili wa afisa wa uhamiaji wa kike, Maude Elliott, kupatikana ukiwa na majeraha makubwa na michubuko katika maeneo ya nyumbani kwake huko Monrovia magharibi mwa Brewerville.
Mwezi Septemba, John Tubman, mtoto wa aliyekuwa rais pia William Tubman, aliuawa na mwili wake kupatikana nyumbani kwake.
Mapema mwaka huu rais George Weah amekosolewa vikali na umma alipowataka kuweka kamera katika nyumba zao ili kujilinda.