Dar es Salaam. Taarifa kwamba serikali ya Marekani inakusudia kuiweka Tanzania kwenye orodha yake ya nchi ambazo raia wake watawekewa vikwazo vya kuingia taifa hilo kubwa duniani, zimeshtua wengi huku maswali ya nini kinaweza kuwa kilisababisha kusudio hilo yakiendelea kuumiza vichwa vya wadadisi.
Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti habari hiyo juzi kwamba uongozi wa Rais Donald Trump unafikiria kuongeza idadi ya nchi ambazo raia wake watawekewa vikwazo vya kuingia nchi hiyo.
Taarifa ya serikali ya Marekani haijataja nchi hizo lakini vyombo vya habari vimebashiri kuwa Tanzania, Eritrea, Nigeria, Belarus, Kyrgyzstan, Myanmar na Sudan zinaweza kuingia katika orodha hiyo.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa Serikali ya Tanzania aliyepatikana jana kuzungumzia suala hilo.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na msemaji wa serikali ya Tanzania kuongelea suala hilo, hazikufanikiwa.
Maofisa wa serikali ya Marekani walivujisha taarifa hiyo ambayo haijathibitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kwa vyombo vya habari kuhusu mpango huo uliodopkezwa na Rais Trump anayehudhuria mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani jijini Davos, Uswisi.
Pia Soma
- Lissu ashtaki Umoja wa Mabunge Duniani
- Binti wa Rais Dos Santos aburuzwa mahakamani
- Alichokisema Lugola baada ya kuambiwa na Magufuli kuwa hafai
Haijajulikana bado ni kwa nini haswa Serikali ya Marekani inakusudia kuweka vizuizi hivyo dhidi ya Tanzania.
Hatua hiyo ya Marekani imeshitua kwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano mzuri kwa miaka mingi.
Ziara ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1963 kwa mwaliko wa rais wa wakati huo wa Marekani, John Kennedy ndio ilikuwa chachu ya uhusiano huo mzuri.
Mwalimu Nyerere alikuwa na ziara nyingine ya kiserikali nchini Marekani mwaka 1977 kwa mwaliko wa Rais Jimmy Carter.
Pia Mwalimu Nyerere alikutana na Rais wa Marekani, Ronaldo Reagan mjini Cancun, Mexico mwaka 1981.
Tanzania pia ilipata bahati ya kutembelewa na marais tofauti wa Marekani, Bill Clinton, George W. Bush na Barrack Obama.
Pia Tanzania imekuwa mnufaika mkubwa wa misaada ya Marekani katika masuala ya kukabiliana na magonjwa hatari kama Ukimwi na kifua kikuu, nishati na uzalishaji chakula.
Taasisi kama PEPFAR, Millennium Challenge, Feed the Future, Global Health Initiative, Power Africa na nyinginezo zimekuwa chachu ya misaada hiyo.
Hata hivyo, tangu kuingia madarakani kwa Rais Trump kumekuwa na mabadiliko makubwa ya sera ya mambo ya nje ya Marekani. Mwaka 2017 iliweka zuio kwa baadhi ya watu nchi za Iran, Libya, Somalia, Syria, Yemen na Korea Kaskazini kwenda nchini humo.
Pia Marekani imebana viongozi wa Venezuela kwenda nchini humo.
Hata hivyo, mahakama kuu za serikali ya shirikisho zimekuwa zikitengua maamuzi hayo kwa sababu tofauti, zikiwemo za ubaguzi wa kidini.
Hata hivyo, haijajulikana mara moja sababu ya Rais Trump kutaka kuweka vikwazo vya utoaji viza kwa nchi hizo saba.
Ingawa jarida la Wall Street Journal la Marekani lilikariri maofisa wa nchi hiyo wakisema si raia wote watakaozuiwa kuingia Marekani, itategemea aina ya viza mathalani kama ni masuala ya biashara au matembezi.
Pia Marekani inataka kufuta mpango wa kuchezesha bahati nasibu kwa raia wa baadhi ya nchi hizo kwa ajili ya kupata viza za kwenda kuishi nchini humo.
Alipoulizwa ni nini kimesababisha nchi yake ifikirie kuchukua uamuzi huo dhidi ya Tanzania, ofisa habari wa ubalozi wa Marekani nchini, Ben Ellis alikataa kujibu maswali kutoka kwa Mwananchi jana.
Hata hivyo, Ellis alikiri kufahamu kuwepo kwa tetesi hizo akisema: “Hatuna kitu chochote cha nyongeza kwa sasa. Hatutaki kupiga ramli.”
Watu tofauti wamekuwa na hisia tofauti kuhusu kusudio hilo, huku baadhi wakitafsiri kuwa ni kutokana na kuwepo madai dhidi ya Serikali ya Tanzania ya kuwepo mapungufu katika masuala ya haki za binadamu na utawala bora wakati wengine wakiuona uamuzi huo kama si wa haki.
Innocent Shoo, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini anadhani kusudio hilo “si wa kawaida na si sawa pia””
“Uamuzi kama huu mara nyingi huchukuliwa dhidi ya nchi ambazo huonekana zinafadhili au kusaidia ugaidi au zina historia mbaya ya haki za binadamu,” alisema.