Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TTCL yaahidi kuendelea kushirikiana na Rwanda

3cf0dc146e9bad929b32d5aee8f98195 TTCL yaahidi kuendelea kushirikiana na Rwanda

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), imeahidi kuendelea kushirikiana kibiashara na nchi ya Rwanda ikiwa ni pamoja na kubadilishana teknolojia na mafunzo katika sekta nzima ya mawasiliano.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Waziri Kindamba, alitoa ahadi hiyo jana mkoani Dar es Salaam baada ya Waziri wa Tehama na Ubunifu wa Rwanda, Paula Ingabire, kutembelea TTCL kwa ajili ya kuendeleza uhusiano.

Alisema TTCL imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano la nchini Rwanda kwa zaidi ya miaka 10 ikiwa ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa intanenti nchini humo.

“Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini Rwanda imepiga hatua kubwa na tutaendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali, lengo ni kuhakikisha sekta hii inaimarika na kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi zetu,” alisema Kindamba.

Kwa upande wake, Waziri Ingabire alisema ziara yake inalenga kuona ni kwa namna gani ushirikiano wa nchi hizi unavyoweza kuendelea kwa kuwa ni wa msingi.

Aidha, alisema watajadili na kuona ni kwa namna gani sekta binafsi katika eneo hilo la mawasiliano, kwenye nchi hizo inavyoweza kufanya kazi kwa pamoja na kuendelea kukuza uchumi wa nchi husika na kuimarisha maendeleo.

Ingabire alisema ipo haja ya kuwa na mfumo wa kubadilishana uzoefu baina ya wataalamu wa nchi hizi kama uti wa mgongo wa kukuza uchumi wa Tanzania na Rwanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, Dk Faustine Ndugulile, alisema nchi ya Rwanda imekuwa na mabadiliko makubwa hasa katika sekta ya mawasiliano, jambo ambalo wanahitaji kuendelea kushirikiana.

Alisema ziara ya waziri huyo inalenga kufika katika Kituo cha Taifa cha Data pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuangalia ni wapi wataboresha zaidi ushirikiano wao.

Chanzo: www.habarileo.co.tz