Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven amtaka Luis aje fasta

90388 Luis+pic Sven amtaka Luis aje fasta

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MABOSI wa Simba walishazungumza na kumalizana kabisa na winga fundi na nahodha wa UD Songo ya Msumbiji, Luis Jose Miquissone, lakini walikuwa wakimsikilizia kocha wao mkuu, Sven Vanderbroek atoe baraka ili aletewe Dar kuja kusaini na kuanza kazi Msimbazi.

Hata hivyo, taarifa tamu kwa mashabiki wa Simba hao ni kwamba kocha huyo amemtaka mchezaji huyo aje jijini Dar es Salaam fasta ili kuliamsha dude kwani ameridhika na kiwango chake cha kusukuma gozi la ng’ombe na anaamini ni mtu anayemhitaji kikosini kwa sasa ili chama likamilike.

Ipo hivi. Kocha Sven alikuwa amepewa wiki mbili na uongozi wa Simba kukifanyia tathmini kikosi hicho na kueleza ubora na mapungufu yake pamoja na mahitaji anayoyataka kwenye dirisha dogo, ila unaambiwa kabla hata wiki ya pili kumalizika jamaa akalipitisha jina Luis bila kizuizi chochote.

Luis alikuwa akifuatiliwa tangu enzi za Kocha Patrick Aussems akishirikiana aliyekuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori kabla ya zigo kuachiwa kwa Mtendaji wa sasa, Senzo Masingiza ambaye inaelezwa kila kitu kilikuwa kimekamilika, lakini hofu ikaja Luis hawezi kusajiliwa na kuletwa Dar kabla ya Sven kumridhia kwa kuhofia kuonekana wanamuingilia kwenye kazi zake.

Unaambiwa sasa, juzi kati Senzo alifanya kikao na Sven cha muda mfupi na kujadili kuhusu Luis kwa kuonyesha video za mechi zake akiwa na UD Songo na zile za timu yake ya taifa ya Msumbiji, ili kama anamfaa kikosini kwake naye baada ya kumchungulia kidogo tu, aliamua kumpitisha fasta.

Inaelezwa kocha huyo kutoka Ubelgiji, aliridhika na kazi anayoifanya Luis uwanjani na kumtaka Senzo na mabosi wa Msimbazi kufanya haraka kumleta Dar ili aanze kazi kwani hana kizuizi naye.

Mwanaspoti lilimsaka Kocha Sven kupata ufafanuzi juu ya taarifa hiyo, naye alikiri ni kweli baada ya kudokezwa juu ya Luis hakutaka mazungumzo yawe marefu kwani alimpitisha na akiamini ni mmoja kati ya wachezaji bora kwa muda aliomwangalia kupitia video zake.

Sven alisema, kabla ya hapo pia alishaona kashkashi za jamaa kupitia mechi za mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika alizozingalia kwenye runinga na kubaini ni bonge la mchezaji anayefaa kuwa naye kikosini.

“Ni mchezaji mzuri anayemudu kucheza wingi zote za kulia na kushoto na pia ana uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho na ukiangalia katika timu yetu tuna wachezaji wa aina yake lakini yeye kuna vitu vimeongezeka kwake na kama tutafanikiwa kumpata haraka katika kipindi hiki litakuwa jambo zuri,” alisema Sven na kuongeza;

“Kama akicheza winga anakuwa na uwezo wa kukimbia kwa kasi eneo la timu pinzani kupitia pembeni ana uwezo wa kupiga krosi na kutoka pasi za kufunga kwa washambuliaji na hata muda mwingine kufunga mwenyewe.”

Alisema kwa jinsi alivyomuona, Luis anapocheza nyuma ya mshambuliaji hutumia kasi yake kupenya ngome ya timu pinzani na kama mabeki wake wasipokuwa makini watamchezea rafu kama ilivyokuwa katika mechi ya pili dhidi ya Simba, pia anatengeneza nafasi za kufunga.

“Luis anaweza kumiliki mpira, ni mzuri wa kupiga mipira iliyokufa (faulo) kama alivyofanya dhidi ya Simba katika mechi ya marudiano ya CAF, kwa maana hiyo atatufaa na kuongeza kitu ndani ya timu jambo lililonifanya nimpitishe bila tatizo,” alisema Sven aliyeiongoza Simba katika mechi tatu na kushinda bila kuruhusu bao.

“Nadhani mpaka kufika Jumanne (kesho) baada ya kucheza mechi yetu na Ndanda ndio nitatoa tathmini yangu kwa ujumla kwa uongozi vitu nilivyoviona na vinavyotakiwa kufanyiwa kazi kikosini, ingawa naona kwa kiwango kikubwa timu imekamilika, ila sehemu chache na pengine tutapunguza baadhi ya wachezaji kwenda kwa mkopo katika timu nyingine,” alisisitiza Sven

Chanzo: mwananchi.co.tz