Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sudan yapinga majeshi ya kigeni kupelekwa nchini humo

Sudan Jeshi Wafungwa.jpeg Sudan yapinga majeshi ya kigeni kupelekwa nchini humo

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sudan imepinga kutumwa wanajeshi wa kigeni nchini humo na kutangaza kuwa itawachukulia wanajeshi hao kuwa ni sawa na askari vamizi.

Tangu Aprili 15, Sudan inashuhudia mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdul Fattah al-Barhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.

Mapigano hayo yamesambaa katika mji mkuu Khartoum na miji mingine ya kaskazini na magharibi mwa nchi.

Mkutano wa jumuiya ya kiserikali ya Afrika Mashariki IGAD ulifanyika siku ya Jumatatu wiki hii katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa ajili ya kuchunguza njia za kumaliza mapigano hayo yanayoendelea nchini Sudan bila ya kuhudhuriwa na ujumbe wa wawakilishi wa jeshi la nchi hiyo.

Washiriki wa mkutano huo wa Addis Ababa waliviomba Vikosi vya Akiba vya Afrika Mashariki (ISAF) kufanya mkutano wa kuangalia uwezekano wa kupeleka askari wake nchini Sudan kusaidia wananchi na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wananchi hao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza katika taarifa kwamba Khartoum haitakubali kamwe kutumwa wanajeshi wa kigeni nchini Sudan, na iwapo watatumwa, wanajeshi hao wa kigeni watachukuliwa kama askari vamizi.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, misaada ya kibinadamu inayotumwa Sudan na mashirika na taasisi za kimataifa inawafikia wahitaji na serikali ya Khartoum imefanya kila juhudi kutatua matatizo ya wananchi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imelaani kauli ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, -ambaye ametaka litengwe eneo la marufuku ya kuruka ndege na zoezi la upokonyaji silaha nzito-, na kusisitiza kuwa Khartoum inayachukulia matamshi hayo kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya utawala wa kitaifa wa Sudan na haikubaliani nayo.

Mwishoni mwa taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeihutubu IGAD kwa kusema: kutoheshimu maoni ya nchi wanachama kutaifanya Khartoum ifikirie upya kuendelea kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo

Chanzo: www.tanzaniaweb.live