Serikali ya Sudan imeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
"Ali Al-Sadiq", Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, aliyekuwa akihutubia kikao cha mabalozi wa kigeni, wajumbe wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ametoa wito wa kukomeshwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo kwa kuzingatia Azimio nambari 1591 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Al-Sadiq amesisitiza kuwa: Hali ya Sudan hii leo ni tofauti kabisa na ile ya mwaka 2005 wakati vikwazo hivyo vilipowekwa.
Akiashiria matukio ya hivi sasa nchini Sudan, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ameiomba jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi za vyama vya siasa vya Sudan kwa ajili ya kupatikana demokrasia na kuandaa njia ya kuondolewa vikwazo.
Vilevile ameeleza matumaini kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakubaliana na ombi la Sudan la kuondoa vikwazo, na amewataka mabalozi wa kigeni kuziarifu serikali zao kuhusu msimamo wa Khartoum.
Vikwazo ilivyowekewa Sudan ni pamoja na silaha, marufuku ya kusafiri na kuzuiwa kwa mali ya watu waliohusika katika mgogoro wa Darfur.