Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa jana yalitoa takwimu mpya na za kutisha yakisema kuwa, watoto laki saba (700,000) nchini Sudan wanakabiliwa na aina mbaya zaidi ya utapiamlo kutokana na vita vya uchu wa madaraka vinavyoendelea baina ya majenerali wa kijeshi nchini humo.
James Elder, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), ameelezea hali mbaya iliyoko nchini Sudan hivi sasa na kusema kuwa inafanana na "uhamisho mkubwa zaidi wa watoto kuwahi kutokea duniani" akisisitiza kuwa, watoto milioni 4 wamelazimika kuyahama makazi yao huko Sudan..
Amesema: "Takwimu zinaonesha kuwa, watoto 13,000 wanahama makazi yao kila siku katika kipindi cha siku 300 zilizopita."
Kwa upande wake, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA hivi karibuni ilitoa mwito wa kutengwa dola bilioni 2.7 za Kimarekani ili kushughulikia mahitaji ya dharura ndani ya Sudan, lakini madola ya kigeni yameshindwa kutoa fedha hizo hadi hivi sasa. Kwa mujiubu wa OCHA ni asilimia nne tu ya fedha hizo ndizo zilizotolewa hadi hivi sasa.
Wahanga wakuu wa vita vya uchu wa madaraka Sudan ni wanawake na watoto wadogo
Haya yanajiri huku vita angamizi vya umwagaji wa damu baina ya majenerali wa kijeshi vikizidi kupamba moto tangu vilipoanza mwezi Aprili 2023. Hali hiyo mbaya inashuhudiwa huku pande zinazopigana nchini Sudan zikishindwa kuonesha ishara zozote za kukomesha vita hivyo vya uchu wa madaraka.
Ziara ya hivi karibu ya James Elder msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) huko Darfur ya Sudan ilifichua mambo ya kutisha na kuhuzunisha. Takwimu za UNICEF zinasema kuwa, zaidi ya watoto 700,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali na UNICEF inaweza kutibu chini ya nusu tu ya watoto hao, hivyo msaada zaidi na wa haraka unahitajika.