Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sudan: Mauaji yaongezeka licha ya mazungumzo

Sudan Update: Bado Mapigano Yanaendelea Omdurman Sudan: Mauaji yaongezeka licha ya mazungumzo

Tue, 9 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Muungano wa Madaktari wa Sudan umeripoti ongezeko la idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika mapigano ya silaha nchini humo licha ya kuendelea juhudi za kuyapatinisha makundi hasimu.

Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kunukuu taarifa ya Muungano wa Madaktari wa Sudan ikisema kwamba, idadi ya waliouawa kutokana na mgogoro wa vita nchini humo imeongezeka na kufikia watu 481.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wengine wasiopungua 2,564 wamejeruhiwa wakati wa mapigano kati ya vikosi vya jeshi na wapiganaji wa msaada wa haraka katika maeneo tofauti ya Sudan.

Hii ni wakati ambapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetangaza kuanza baadhi ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa pande hizo hasimu mjini Jeddah. Vita vya kuwania madaraka vimesababisha maafa makubwa nchini Sudan

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC yenye nchi wanachama 57, hivi karibuni ilitoa taarifa na kutangaza kuwa Hossein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, ameziomba nchi wanachama wa taasisi za kifedha na kibinadamu kupeleka misaada yao haraka nchini Sudan.

Taarifa hiyo ilisema: Hali ya kibinadamu nchini Sudan ambayo kwa miaka mingi imekumbwa na mgogoro mkubwa, imezidi kuwa mbaya hivi sasa na msaada wa haraka wa kibinadamu unahitajia kuokoa roho za mamilioni ya watu nchini humo.

Kabla ya hapo, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alinukuu taarifa ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ikisema kuwa kuendelea mgogoro wa hivi sasa nchini Sudan kutasababisha zaidi ya watu milioni 19 kukumbwa na njaa na utapiamlo mkali katika miezi ijayo nchini humo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live